• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 22, 2018

  TFF HAIJAFURAHIA YANGA KUFIKA MBALI KWENYE MICHUANO YA AFRIKA MWAKA HUU?

  KAULIMBIU ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais Wallace Karia ni; “Play Fair, Be Positive” ambayo tafsiri yake halisi ni “Cheza Kiungwana na Kuwa Chanya”, yaani usiwe mtu wa kupinga pinga.
  Hapana shaka, dhamira ya kaulimbiu hiyo ni kukumbushana umuhimu wa mchezo wa kiungwana, ambayo pia ni kauli mbiu kuu ya wenye mpira wao, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), lakini pia kuambiana kuwa na desturi ya kuunga mkono hususan yale yanayoonekana ni chanya.
  Kama FIFA wanasema Fair Paly (Mchezo wa Kiungwana) na TFF wanakuja na kaulimbiu ya Play Fair, Be Positive hii inatuaminisha huu ni mwanzo wa zama mpya katika soka ya
  Tanzania ambazo haswa zilikuwa zinasubiriwa.
  Tunahitaji mchezo wa kiungwana kwa kila mtu miongoni mwetu, kuanzia viongozi wa TFF, klabu, vyama shiriki vikiwemo vya mikoa na wilaya, wachezaji, waamuzi, wana Habari na wadau wote kwa ujumla ili kuipata maana halisi ya Play Fair.
  Lakini pia tunahitaji kuwa chanya kuwa kuacha desturi ya kupinga pinga mambo tu kwa sababu tunapenda kuwa tofauti wakati wote kwa kupinga hata yale ambayo si hasi na yenye tija kwa soka ya Tanzania.
  Lakini ajabu hali ilivyo katika soka ya Tanzania haionyeshi kama inaakisi maana halisi ya Play Fair, Be Positive na kinachoonekana ni kama sheria ipo, au zipo lakini inachagua pa kufanya kazi katika misingi ya haki na kwingine mambo yanakwenda kwa utashi maalum.
  Mapungufu makubwa yanaonekana katika uchezeshaji wa marefa kwenye mechi za Ligi Kuu zinazoendelea nchini, iwe kwa bahati mbaya au vyovyote lakini pamoja na kwamba kanuni zipo wazi, hatuoni wanachukuliwa hatua.
  Lakini marefa wengine kwa makosa unayoweza kuyaita madogo na unayoweza kuyatetea kama ya kibinadamu wamekuwa wakiadhibiwa, tena vikali.
  Kwa ujumla, Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi ya Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72 imekuwa na mapungufu mengi na makubwa – zaidi kuchelewa kufanya vikao vyao kupitia taarifa mbalimbali za mechi kabla ya kuchukua hatua.
  Kwa kawaida mchezaji anatakiwa kuanza kutumikia adhabu mara tu baada ya kutenda kosa, lakini tumeshuhudia katika Ligi yetu mchezaji akiendelea kucheza baada ya kufanya kosa tu kwa sababu Kamati ya Saa 72 haijaketi kupitia taarifa.
  Lakini wachezaji wengine wamekuwa wakipelekwa barua ya kusimamishwa kwa muda usiojulikana hata kabla ya Kamati haijaketi kupitia taarifa – japo baadaye huadhibiwa kweli, ambayo inaleta ukakasi kwa sababu wanaanza kutumikia adhabu kabla ya hukumu.
  Kipa wa Azam FC, Mghana Razack Abalora alidaiwa kufanya makosa katika mechi dhidi ya Simba SC Februari 7 mwaka huu, lakini akadaka kwenye mechi mbili zilizofuata dhidi ya Kagera Sugar Februari 11 na Lipuli Februari 16, kabla ya kuletewa barua ya kusimama kabla ya mechi na Singida United Machi 3 na baadaye akafugiwa mechi tatu.
  Dunia nzima hii inatokea Tanzania tu, ambako mchezaji haanzi kutumikia adhabu mara tu baada ya kosa laketu kwa sababu Kamati haijakutana. 
  Katika dunia ya leo ya sayansi na teknolojia, tena ya hali ya juu ni jambo la fedheha mno kwa Kamati ya Saa 72 kuchelewa kufanya vikao vyake kwa nana yoyote kupitia taarifa za mechi ili kuchukua hatua stahili.
  Lakini pia maana halisi ya Neno Kamati ya Saa 72 imekuwa inapotoshwa na ucheleweshaji wa vikao vya kupitia taarifa za waamuzi.
  Pamoja na hayo, Bodi ya Ligi nayo imekuwa na maamuzi fulani ya kibabe wakati fulani, bila kuzingatia maslahi ya moja kwa moja ya taifa, kwa mfano kuzibananisha timu zinazoshiriki michuano ya Afrika kwenye ratiba ya Ligi Kuu.
  Mfano Yanga ilirejea nchini Alhamisi karibu saa nane usiku kutoka Ethiopia ambako ilifanikiwa kuitupa nje Wolaita Dicha na kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, lakini imelazimishwa kwenda kucheza mechi ya Ligi Kuu Mbeya leo, tu kwa sababu eti isiwe na viporo vingi.
  Yanga imecheza Jumatano, imeondoka Ethiopia Alhamisi imefika sawa tu na Ijumaa na Jumamosi imesaifri kwenda Mbeya kwa ajili ya mechi ya leo – hivi wakilalamika hawatendewi haki tunaweza kukataa vipi?
  Klabu zinacheza michuano ya nyumbani ili kupata nafasi ya kucheza michuano ya Afrika – na kama haziwezi kupewa fursa nzuri ya kushiriki michuano hiyo zinazoipigania msimu mzima hapa Tanzania, ina maana gani?
  Yapo mambo hayawezi kukwepeka, lazima Bodi ya Ligi izingatie hilo – kama Yanga wapo kwenye michuano ya Afrika ambayo kalenda yake inaingiliana na Ligi Kuu, lazima wapewe nafasi.
  Au TFF na Bodi ya Ligi hazipendi kuona timu klabu zetu zinafika mbali kwenye michuano ya Afrika ili sizivuruge ratiba ya Ligi na mashindano ya nyumbani kwa ujumla – na kama ni hivyo, tuamini hawajafurahi Yanga kuingia hatua ya makundi kwa sababu sasa wataongeza idadi ya viporo katika Ligi Kuu? 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TFF HAIJAFURAHIA YANGA KUFIKA MBALI KWENYE MICHUANO YA AFRIKA MWAKA HUU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top