• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 24, 2018

  KOCHA MKONGO AWASILI KUCHUKUA NAFASI YA LWANDAMINA YANGA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), yupo mjini Dar es Salaam kwa ajili ya mipango ya kujiunga na klabu ya Yanga.
  Taarifa ambazo Bin Zubeiry Sports – Online imezipata kutoka Yanga zinasema kwamba kocha huyo anatarajiwa kuondoka leo Dar es Salaam kwenda Morogoro ambako kikosi cha timu hiyo kimeweka kambi kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu, Simba SC.
  Mwinyi alikuwa kwenye benchi la Ufundi la timu ya taifa ya DRC, The Leopard na uzoefu wa kufundisha soka hadi Ulaya, nchini Ufaransa.
  Mwinyi Zahera yupo Dar es Salaam kukamilisha mipango ya kujiunga na klabu ya Yanga

  Hii inamaanisha Yanga imeamua kuachana moja kwa moja na kocha wake, George Lwandamina aliyeondoka wiki mbili zilizopita kurejea kwao, Zambia kukamilisha mipango ya kujiunga tena na klabu yake ya zamani, Zesco United.    
  Zahera anakuja Yanga akitokwa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako alikuwa Msaidizi wa Florent Ibenge tangu Sep 30, mwaka jana.
  Lakini Zahera pia amezifundisha DC Motema Pembe ya kwao, DRC tangu Machi 1, mwaka 2015 hadi Machi 10, 2016, akitoka kuwa kaimu kocha wa AFC Tubize ya Ubelgiji kati ya Oktoba 7 na Oktoba 23, mwaka 2014 ambayo alijiunga nayo akitoka kuwa Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya DRC kati ya Agosti 14 na 28, mwaka 2017 chini ya Ibenge.
  Alikuwa anafundisha AFC Tubize kwa mara ya pili, baada ya awali kuifundisha kama Kocha Mkuu kuanzia Julai 1 hadi Oktoba 20, mwaka 2010.
  Zahera Mwinyi alizaliwa Oktoba 19, mwaka 1962 kabla ya kuanza soka mwaka 1975 akiichezea klabu ya Bankin ya Goma, Kaskazini mwa jimbo la Kivu, DRC hadi mwaka 1980.
  Baadaye akaenda Kinshasa kucheza soka na kujiendeleza kielimu, akijiunga na Chuo cha Teknolojia (ISTA) huku akichezea klabu ya Sozacom hadi alipokutana na wakala wa wachezaji, Mbelgiji Karl Broken aliyemchukua na kumpeleka Ulaya kucheza soka ya kulipwa.
  Mwinyi Zahera alicheza kwa misimu miwili Antwerp FC ya Ubelgiji kabla ya kumaliza mkataba wake na kwenda Ufaransa alikochezea timu za Daraja la Pili, Amiens, Beauvais na Abbeville hadi akastaafu soka.
  Baada ya hapo akaanza kupata mafunzo ya ukocha, Zahera Mwinyi ambako alitunukiwa Diploma na leseni A ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) kabla ya kuifundisha klabu ya SC Feignies ya Ufaransa kuanzia mwaka mwaka 2000 hadi 2010 kwa mafanikio makubwa kabla ya kwenda Ubelgiji kuifundisha Tubize na baadaye jkutrejea nyumbani, DRC na sasa amekuja kujaribu maisha mapya Tanzania.
  Lwandamina alijiunga na Yanga Novemba mwaka 2016 akichukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na katika kipindi hicho ameiongoza timu katika michezo 77 ya mashindano yote akitoa sare 18, kushinda 45 kati ya hizo mbili kwa penalti baada ya sare ndani ya muda wa kawaida na kufungwa 14, tano kwa penalti baada ya sare katika muda wa kawaida.
  Na tangu aondoke, klabu imebaki chini ya makocha waliokuwa wasaidizi wake, Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazawa, Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali ambaye ni kocha wa makipa.
  Kwa sasa kikosi cha Yanga kipo kambini mjini Morogoro kikijiandaa na mchezo dhidi ya Simba Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
  Simba SC iliyo chini ya kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mtunisia, Aymen Mohamed Hbibi, Mrundi, Masoud Juma na mzawa Muharami Mohamed ‘Shilton’ inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 59 baada ya kucheza mechi 25, wakati Yanga inafuatia kwa mbali kidogo ikiwa na pointi zake 48 za mechi 23.
  Yanga inazidiwa pointi 11 na Simba SC na ina viporo viwili, maana yake ili kutetea ubingwa wao, itabidi washinde Jumapili na washinde mechi zao zote zilizobaki za Ligi Kuu, huku wakiwaombea mahasimu wao hao wapoteze mechi nyingine pia moja – jambo ambalo hakika ni gumu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KOCHA MKONGO AWASILI KUCHUKUA NAFASI YA LWANDAMINA YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top