• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 21, 2018

  SAMATTA ACHEZA DAKIKA NANE TU GENK YASHINDA 2-1 UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku huu amecheza kwa dakika nane tu, klabu yake, KRC Genk ikishinda 2-1 dhidi ya Anderlecht katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
  Ushindi huo umetokana na mabao ya washambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Dieumerci N'Dongala dakika ya pili na Mbelgiji Leandro Trossard dakika ya 59, wakati bao la wageni lilifungwa na kiungo Mserbia, Lazar Markovic dakika ya 20.
  Samatta akainuliwa dakika ya 82 kwenda kuchukua nafasi ya mshambuliaji wa kimataifa wa Ugiriki, Nikolaos Karelis kumalizia dakika nane za mwisho na kuisaidia Genk kushinda.
  Mbwana Samatta leo amecheza kwa dakika nane tu Genk ikishinda 2-1 Ligi ya Ubelgiji

  Hiyo inakuwa mechi ya 84 kwa Nahodha huyo wa Taifa Stars, Samatta tangu alipojiunga na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 
  Na katika mechi hizo, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano yote.
  Kikosi cha KRC Genk kilikuwa; Vukovic, Nastic, Colley, Aidoo, Maehle, Seck, Malinovskyi, Pozuelo, Trossard/Buffel dk90+1, Ndongala/Mata dk85 na Karelis/Samatta dk82.
  RSC Anderlecht; Sels, Sa, Gerkens, Saif, Kums/Morioka dk67, Trebel, Dendoncker, Obradovic, Markovic/Amuzu dk79, Saelemaekers/Bruno dk67 na Teodorczyk.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA ACHEZA DAKIKA NANE TU GENK YASHINDA 2-1 UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top