• HABARI MPYA

    Friday, April 27, 2018

    SIMBA YAWATISHA WATANI; “TUKO KAMILI NA HATUNA MAJERUHI HATA MMOJA”

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imesema haina majeruhi hata mmoja kikosini kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao, Yanga Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Simba wakiwa vinara wa ligi hiyo kwa pointi 59 kutokana na mechi 25, watakuwa wenyeji wa mchezo huo dhidi ya Yanga waliopo nafasi ya pili na pointi 48, huku wakiwa wameshuka dimbani mara 23.
    Timu hizo ziliweka kambi mjini Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao, Simba wamerejea jana na kuendelea na mazoezi yao katika Uwanja wa Boko Veterani nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
    Nahodha John Bocco (kulia) na beki Shomari Kapombe wako fiti kuelekea mchezo wa leo

    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Hajji Manara amesema kwamba maandalizi yanaendelea vizuri baada ya kikosi cha timu hiyo kurejea wakitokea Morogoro walipoweka kambi ya siku tatu.
    Amesema taarifa kutoka benchi la ufundi kwamba kikosi hicho kinaendelea vizuri na tayari kwa ajili ya mchezo huo kwa kuhakikisha wanapata pointi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya mbio za ubingwa.
    “Hadi leo hatuna majeruhi na timu inaendelea na mazoezi yake, kikubwa tunawaomba waamuzi kuzitendea haki kanuni na sheria za soka, waepuke kuingia na matokeo yao,
    “Tunahitaji matokeo kwa kila mechi, kikubwa ni kupata pointi muhimu zitakazotufanya tukaendelea kubaki katika nafasi tuliyopo, kwa kufanikiwa kutwaa Ubingwa,” amesema.
    Manara amesema anaiheshimu Yanga haswa kuelekea katika pambano hilo la watani wa jadi, hivyo huenda wasipate ushindi ila wanaenda kutafuta pointi muhimu katika mchezo huo.
    “Tuna imani ya kuchukuwa ubingwa, lakini sio kama tutashinda mechi zote, mashabiki watambue kwamba kuna mechi tutapoteza, lakini kikubwa vijana wanapambana kuhakikisha tunafikia malengo yaliyokuwepo tangu awali,” amesema Manara.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAWATISHA WATANI; “TUKO KAMILI NA HATUNA MAJERUHI HATA MMOJA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top