• HABARI MPYA

  Jumatatu, Aprili 23, 2018

  TAMBWE AINGIA KAMBINI YANGA KUANZA KUIPASHIA SIMBA MECHI YA JUMAPILI TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Mrundi wa Yanga, Amissi Jeselyn Tambwe ameingia kambini leo mjini Morogoro kujiandaa kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wa jadi, Simba SC.
  Zote, Simba na Yanga zimeamua kuweka kambi katika mji wa Morogoro kujiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumapili wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Simba wapo Morogoro tangu jana, walipowasili wakitokea Iringa ambako Jumamosi walicheza mechi nyingine ya Ligi Kuu na kulazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, Lipuli Uwanja wa Samora.
  Mahasimu wao, Yanga wapo njiani wakikaribia kufika Morogoro pia tayari kuweka kambi kwa ajili ya mchezo wao huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
  Amissi Tambwe (kushoto) ameingia kambini leo mjini Morogoro kujiandaa na mechi dhidi ya Simba SC Jumapili

  Lakini Tambwe na beki Andrew Vincent ‘Dante’ na kiungo mshambuliaji, Ibrahim Ajib wanatokea Dar es Salaam jioni hii wakiongozana na Meneja, Hafidh Saleh kwenda kuungana na wenzao wanaotokea Morogoro.
  Tambwe, Dante na Ajib wote hawa kusafiri na timu kwenda Mbeya ambako jana Yanga ililazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, Mbeya City katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu kutokana na kuwa majeruhi, wakati Meneja Saleh amerejea jana kutoka Cairo, Misri alipokwenda kuiwakilisha klabu kwenye upangwaji wa makundi ya Kombe la Shirikisho.
  Tambwe, Dante na Ajib hawakwenda pia Ethiopia kwenye mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, ambako Yanga ilifungwa 1-0 Jumatano mjini Hawassa na kufuzu kwa ushindi wa jumla wa 2-1 baada ya awali kushinda 2-0 Dar es Salaam. 
  Katika mchezo wa Jumapili, Simba watahitaji kushinda ili kujisafishia njia ya ubingwa, wakiwa sasa wanaongoza kwa pointi zao 59 baada ya kucheza mechi 25, wakati Yanga inafuatia kwa mbali kidogo ikiwa na pointi zake 48 za mechi 23.
  Yanga inazidiwa pointi 11 na Simba SC na ina viporo viwili, maana yake ili kutetea ubingwa wao, itabidi washinde Jumapili na washinde mechi zao zote zilizobaki za Ligi Kuu, huku wakiwaombea mahasimu wao hao wapoteze mechi nyingine pia moja – jambo ambalo hakika ni gumu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TAMBWE AINGIA KAMBINI YANGA KUANZA KUIPASHIA SIMBA MECHI YA JUMAPILI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top