• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 20, 2018

  AISHI MANULA, OKWI WAIPA WAKATI MGUMU SIMBA KUELEKEA MECHI NA LIPULI KESHO SAMORA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC ipo Iringa tangu jana, tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Lipuli kesho Uwanja wa Samora, lakini kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anaumiza kichwa juu ya kipa Aishi Salum Manula na mshambuliaji Emmanuel Arnold Okwi kuwachezesha au kutowachezesha kesho. 
  Wawili hao, kipa namba moja wa Tanzania na mshambuliaji tegemeo wa Uganda kila mmoja tayari ameonyeshwa kadi mbili za njano na kama atawachezesha kesho na bahati mbaya wakaonyeshwa tena kadi, maana yake watakosekana kwenye mechi dhidi ya mahasimu, Yanga Aprili 29, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Lakini wakati huo huo wawili hao wamekuwa muhimu mno katika kampeni za Simba SC kutwaa taji la kwanza la ubingwa wa Ligi Kuu baada ya miaka sita na Lechantre anayesaidiwa na Mtunisia, Aymen Mohammed Hbibi, Mrundi Masoud Juma na mzawa, Muharami Mohammed ‘Shilton’ anahofia kuwatumia huku akihitaji kuwatumia.
  Aishi Manula ana kadi mbili za njano sawa na Emmanuel Okwi (chini kulia) kuelekea mechi na Lipuli na kesho 

  Lechantre anatarajiwa kufanya maamuzi ya mwisho baada ya mazoezi ya leo jioni Uwanja wa Samora mjini Iringa, kwa sababu japokuwa kipa wa pili, Said Mohammed ‘Nduda’ yupo fiti, lakini hajadaka mechi hata msimu huu.
  Na Okwi ndiye amekuwa injini ya Simba SC akiwa amefunga mabao 19 msimu huu katika Ligi Kuu pekee, akiisaidia timu hiyo kuwa kileleni kwa pointi zake 58 za mechi 24, mbele ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 47 za mechi 22. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AISHI MANULA, OKWI WAIPA WAKATI MGUMU SIMBA KUELEKEA MECHI NA LIPULI KESHO SAMORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top