• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 28, 2017

  MKAGUZI WA CAF AAFIKI YANGA NA MC ALGER ZICHEZE KIRUMBA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MKAGUZI wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Maxwell Mtonga kutoka Malawi ameridhia mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shierikisho Afrika kati ya wenyeji, Yanga SC na MC Alger ya Algeria uchezwe Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Aprili 8, mwaka huu baada ya marekebisho madogo aliyoelekeza.  
  Mtonga yupo Mwanza tangu juzi akiongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi katika ukaguzi huo na ameagiza marekebisho madogo madogo.
  Mkaguzi wa CAF, Maxwell Mtonga (wa pili kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi (katikati) na Maofisa wengine wakati wa ukaguzi Uwanja wa CCM Kirumba leo 

  Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba, Steven Shijja amesema watahakikisha wanafanya marekebisho hayo ndani ya muda kama walivyoelekezwa na mchezo huo utafanyika Mwanza bila shaka 
  Viongozi wa Yanga wapo katika harakati za kufanikisha mpango wa kuuhamishia mchezo huo Mwanza kutoka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa matarajio ya kupata watazamaji wengi na pato kubwa.
  Tayari mchezo wa Ligi Kuu ya Vodaocm Tanzania Bara kati ya wenyeji Mbao FC na Simba SC ya Dar es Salaam uliokuwa ufanyike Aprili 8, mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba, umesogezwa mbele kwa siku mbili hadi Aprili, 10.
  Lakini taarifa ya Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura jana ilisema kwamba hatua hiyo imechukuliwa ili kupisha shughuli za kijamii kwenye Uwanja huo zitakazoanza Aprili 1 hadi 9.
  Yanga SC imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Zanaco Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia ikitoka kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MKAGUZI WA CAF AAFIKI YANGA NA MC ALGER ZICHEZE KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top