• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 30, 2017

  MBARAKA YUSSUF AWAAMBIA SIMBA; “HAKUNA KUCHEKEANA JUMAPILI”

  Na Mahmoud Zubeiry, BUKOBA
  MSHAMBULIAJI chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Mbaraka Yussuf Abeid anayechezea Kagera Sugar ya Bukoba ameiambia klabu yake ya zamani, Simba SC hakuna kujuana Jumapili Uwanja wa Kaitaba mjini hapa.
  Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Simba SC Jumapili Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Bara na Mbaraka amesema kwamba siku hiyo hakuna kuchekeana.
  “Ni kweli mimi Simba ni timu yangu ya zamani, lakini kwa sasa mimi ni mchezaji wa Kagera Sugar. Nina wajibu wa kumfurahisha mwajiri wangu na mashabiki wa Kagera na wakazi wa mkoa Bukoba kwa ujumla,”alisema jana akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online.
  Mbaraka Yussuf (kulia) ameiambia klabu yake ya zamani, Simba SC hakuna kujuana Jumapili Uwanja wa Kaitaba  

  Pamoja na hayo, mchezaji huyo aliyeibuliwa kikosi cha vijana cha Simba kabla ya kuhamia Kagera Sugar msimu uliopita, alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu kila timu ipo vizuri.
  Mbaraka alisema kwamba wanaiheshimu Simba ni timu kubwa ina mashabiki wengi kila sehemu, lakini wao Kagera Sugar wanataka pointi katika mchezo wa Jumapili.
  “Na sisi tunataka kushinda tupate pointi tatu, haijalishi tunagombea ubingwa au nafasi ya pili, kikubwa ni kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri katika Ligi,”alisema.
  Mbaraka aliwasili Bukoba jana asubuhi kujiunga na timu yake kwa ajili ya mchezo wa Aprili 2, baada ya kukosekana kwa zaidi ya wiki kufuatia kuitwa kwenye kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu msimu huu akiwa mmoja wa vinara wa mabao.
  Na chipukizi huyo baada ya kuwa benchi muda wote Stars ikiifunga Botswana 2-0 Jumamosi, akaingizwa kipindi cha pili katika mchezo dhidi ya Burundi Jumanne na kufunga bao la ushindi dakika ya 77, Tanzania ikishinda 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MBARAKA YUSSUF AWAAMBIA SIMBA; “HAKUNA KUCHEKEANA JUMAPILI” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top