• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 24, 2017

  TAIFA STARS ITAVUNA NINI KWA MAYANGA?

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kesho inatarajiwa kucheza mchezo wa kwanza chini ya kocha mpya, Salum Yanga wakati itakapomenyana na Botswana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mayanga ameita wachezaji 26 kwa ajili ya mchezo huo na wa Jumanne dhidi ya Burundi, ambayo ni sehemu ya maandalizi ya kufuzu michuano ya CHAN  AFCON. 
  Mayanga aliyempokea Charles Boniface Mkwasa, amefanya mabadiliko madogo katika kikosi hicho kutoka kile kilichokuwa chini ya mtangulizi wake huyo.
  Hajawajumuisha wachezaji kama mabeki Juma Abdul, Kevin Yondan wa Yanga, Aggrey Morris, David Mwantika wa Azam na mshambuliaji Elias Maguli anayecheza Oman.
  Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam

  Lakini kikosini ana wachezaji wapya kabisa, washambuliaji chipukizi, Mbaraka Yussuf wa Kagera Sugar na Abdulrahman Juma wa Ruvu Shooting. 

  Amemkosa mchezaji mmoja tu kati ya 26 aliowaita, ambaye ni Thomas Emanuel Ulimwengu wa AFC Eskilstuna ya Sweden.
  Mayanga pia amebadili benchi la Ufundi, akimuondoa Peter Manyika katika nafasi ya kocha wa makipa na kumchukua rafiki yake, Patrick Mwangata.
  Amemtema Meneja Omar Kapilima na kumchukua Danny Msangi, amemuacha Mtunza Vifaa Hussein Swedi ‘Gaga’ na kumchukua Ally Ruvu, wakati Madaktari wanaendelea kuwa Richard Yomba na Gilbert Kigadya.
  Taifa Stars itaanza na Rwanda katika kuwania tiketi ya CHAN mwakani nchni Kenya na mechi ya kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kati ya Julai 14 na 16 kabla ya timu hizo kurudiana Uwanja wa Amahoro, Kigali kati ya Julai 21 na 23.
  Ikifanikiwa kuitoa Rwanda, Tanzania itamenyana na mshindi kati ya Uganda na ama Sudan Kusini au Somalia katika Raundi ya Tatu ya mchujo mechi ya kwanza ikichezwa kati ya Agosti 11, 12 na 13 na marudiano kati ya Agosti 18, 19 na 20, mwaka huu.
  Tanzania imewahi kushiriki mara moja tu fainali za CHAN, ambayo ilikuwa ni mwaka 2009 zikifanyika kwa mara ya kwanza kabia nchini Ivory Coast na kutolewa katika hatua ya makundi.
  Kwa upande wa AFCON, Taifa Stars imepangwa Kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho.
  Mshindi wa kila kundi atafuzu moja kwa moja AFCON ya 2019, wakati timu nyingine tatu zitakazomaliza nafasi ya pili na wastani mzuri zaidi ya nyingine zitafuzu kama washindi wa pili bora. 
  Tanzania imewahi kucheza mara moja tu fainali za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilitolewa hatua ya makundi pia. 
  Ikumbukwe, hii ni mara ya pili kwa Mayanga kuwa katika benchi la Ufundi la Taifa Stars, baada ya awali kuwa Msaidizi wa Mholanzi, Mart Nooij kwa mwaka mmoja hadi Juni mwaka juzi walipoondolewa kwa matokeo mabaya na Mkwasa kupewa timu. 
  Haijulikani TFF imegundua nini hadi kumrejesha Mayanga Taifa Stars baada ya Mkwasa pia aliyeunda timu pana ya benchi la Ufundi ikimjumuisha gwiji, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ kufeli.
  Idadi kubwa ya wachezaji ni wale wale, ambao Mayanga alikuwa nao akiwa Msaidizi wa Nooij, ukiondoa wapya wachache kama Kabunda, Mbaraka na Abdulrahman.
  Je, Watanzania watarajie nini kutoka Taifa Stars ya Mayanga, mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar aliyewahi pia kufundisha timu za vijana za taifa na klabu za Mtibwa, Prisons na Kagera Sugar?
  Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona kuanzia Jumamosi kwenye mchezo na Botswana. Karibu tena Mayanga Taifa Stars na kila la heri.   

  Salum Mayanga (kulia) wakati akiwa Msaidizi wa Mart Nooij (kushoto)


  Kikosi cha Taifa Stars ya Mayanga
  Makipa; Aishi Manula (Azam FC), Deogratius Munishi (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
  Mabeki; Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael (Azam FC), Vincent Andrew (Yanga SC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Erasto Nyoni (Azam FC).
  Viungo; Himid Mao (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC), Frank Domoyo (Azam FC) na Muzamil Yassin (Simba), Simon Msuva (Yanga SC), Shizza Kichuya (Simba SC), Farid Mussa (Tenerife, Hispania) na Hassan Kabunda (Mwadui FC).
  Washambuliaji: Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Ibrahim Hajib (Simba SC), Mbaraka Yussuf (Kagera Sugar) na Abdul-Rahman Mussa (Ruvu Shooting).
  Benchi la Ufundi; Salum Mayanga (Kocha Mkuu), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja wa Timu), Ally Ruvu (Mtunza Vifaa), Richard Yomba (Daktari) Gilbert Kigadya (Dakati wa Viungo).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TAIFA STARS ITAVUNA NINI KWA MAYANGA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top