• HABARI MPYA

    Friday, March 24, 2017

    SAMATTA: WAZOEFU HAWAJAWA NA MSAADA TAIFA STARS

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta, amesema kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakitumika wachezaji wazoefu kwenye timu hiyo, lakini mafanikio hayajapatikana.
    Akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari katika hoteli ya Urbun Rose, eneo la Kisutu, Dar es Salaam leo mchana, Samatta alisema kwamba ni kwa sababu hiyo kocha mpya, Salum Mayanga ameamua kubadilisha kikosi.
    “Kwa muda mrefu wachezaji wazoefu wamekuwa wakitumika katika nchi hii, lakini timu ya taifa haijapata mafanikio yoyote. Mimi naona tuunge mkono tu mabadiliko yaliyofanywa na kocha,”amesema Samatta.
    Mbwana Samatta amesema kwa muda mrefu wachezaji wazoefu hawajaweza kuiletea mafanikio Taifa Stars

    Mshambuliaji huyo wa KRC Genk ya Ubelgiji, amesema kila mchezaji wa Tanzania ana haki ya kuichezea timu ya taifa, hivyo mabadiliko yaliyofanywa na Mayanga kuwapa nafasi wengine si mabaya.
    Kuelekea mchezo wa kesho wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Botswana, Samatta amesema kama timu Taifa Stars wako tayari na wanatarajia matokeo mazuri.
    “Tuko vizuri na tuko tayari kwa ajili ya mchezo huo. Tunatarajia utakuwa mchezo mgumu kwa sababu tunacheza na timu ya taifa ya wenzetu ambao wamejipanga pia. Lakini kwa sababu tutakuwa nyumbani, tunatarajiwa matokeo mazuri,”amesema.
    Awali ya hapo, kocha Mayanga alizungumzia mchezo huo na akasema anatarajia kuutumia kujua mapungufu ya kufanyia kazi kabla ya kuingia kwenye mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zinazohusisha wachezaji wanaocheza Ligi za nchini mwao pekee. 
    “Ni michezo muhimu, ambayo tunatarajia itatupa mwanga mzuri wa maandalizi yetu kabla ya mechi za kufuzu AFCON na CHAN,”alisema Mayanga aliyeongozana pia na Manahodha Wasaidizi, Jonas Mkude wa Simba na Himid Mao wa Azam. 
    Mayanga pia alifurahia kuwasili kwa mchezaji mwingine anayecheza Ulaya, Farid Mussa aliyetua nchini usiku wa kuamkia leo na akasema atamtumia katika mchezo wa kesho. “Nimepata wachezaji wawili wanaocheza Ulaya, nimemkosa mmoja tu (Thomas Ulimwengu wa AFC Eskilstuna) ambaye hayuko fiti,”alisema.
    Naye kocha wa Botswana, Muingereza Petter Buffer alisema amekuja na kikosi kizuri kikiongozwa na Nahodha, Ofendse Nato anayecheza India na anatarajia pia matokeo mazuri.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas kwa upande wake alitajan viingilio vya mchezo huo kuwa ni Sh. 3,000 kwa majukwaa ya rangi ya chungwa, bluu na kijani, wakati VIP B itakuwa Sh. 10,000 na VIP A Sh. 15,000. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA: WAZOEFU HAWAJAWA NA MSAADA TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top