• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 30, 2017

  SERENGETI BOYS WAIPIGA 3-0 BURUNDI KAITABA

  Na Mahmoud Zubeiry, BUKOBA
  TIMU ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Burundi jioni ya leo Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na fainali za vijana Afrika Mei mwaka huu nchini Gabon.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mtanzania, mwenye beji ya FIFA, Deonisya Rukyaa, wenyeji walikwenda kupumzika wakiwa wanaongoza 2-0.
  Mabao hayo yalifungwa na kiungo Muhsin Makame na beki wa kushoto, Nickson Kibabage aliyepanda kusaidia mashambulizi.
  Makame alifunga dakika ya 19 akimalizia pasi ya Israel Mwenda kutoka upande wa kulia, wakati Kibabage alifunga dakika ya 38 baada ya kupanda na mpira upande wa kushoto na kuingia nao ndani kabla ya kumtungua kipa Djuma Bitiyaweho.
  Pamoja na wenyeji kurudi vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa wanaongoza kwa mabao 2-0, lakini timu hizo zilishambulkiana kwa zamu na labda tu Burundi walikwamishwa na uimara wa safu ya ulinzi ya Tanzania.
  Nahodha Kevin Nashon Naftali (kushoto) akishangilia baada ya kuifungia bao la tatu Serengeti Boys

  Kipindi cha pili nyota ya vijana wa kocha Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ anayesaidiwa na Mshauri wa Ufundi, Kim Poulsen kutoka Denmark, iliendelea kung’ara baada ya kufanikiwa kupata bao la tatu, lililofungwa na Nahodha Kevin Nashon Naftali dakika ya 72.
  Naftali alifunga bao hilo kwa penalti, baada ya beki mmoja wa Burundi kuunawa mpira uliopigwa na beki wa kushoto, Nickson Kibabage.
  Serengeti Boys iliendelea kucheza vizuri kwa kushambulia kusaka mabao zaidi, lakini waliishia kupoteza nafasi. 
  Timu hizo zitarudiana Jumamosi Uwanja wa Kaitaba, kabla ya Serengeti kupanda ndege kwenda Darves Salaam kucheza na U-17 ya Ghana Jumatatu.
  Asad Juma Ali akimiliki mpira mbele ya mchezaji wa Burundi

  Muhsin Makame wa Tanzania akiwatoka wachezaji wa Burundi


  Shaaban Zubeiry Ada akimtoka mchezaji wa Burundi
  Kikosi cha Serengeti kitaondoka Jumatano kwenda Morocco kwa kambi rasmi ya mwezi mmoja ya maandalizi ya fainali za U-17 Gabon zinazotarajiwa kuanza Mei 14.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Dickson Nickson, Israel Mwenda, Nickson Kibabage, Henrick Nkosi, Ally Ng’anzi, Shaaban Zubeiry, Muhsin Makame, Asad Ally, Kevin Naftali na Yohana Nkomola/Ibrahim Abdallah dk79.
  Burundi; Djuma Bitiyaweho, Omar Nzeyimana, Paul Amayungo, Djuma Ndayisenga, Blandin Muhimpundu, Simon Akabeza, Hugue Ininahazwe/Pierre niyonkuru dk60, Jean Noel Nzoyiha/Angelo Buberintwari dk46, Theodore Ngabirano/Fiston Uwizeye dk85, Akbar Asumani/Djuma Minani dk59 na Frank Nzojibwami.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS WAIPIGA 3-0 BURUNDI KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top