• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 24, 2017

  MKUDE: MECHI HIZI ZITAMPA DIRA KOCHA MAYANGA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  NAHODHA Msaidizi wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Jonas Mkude amesema kwamba mechi mbili mfululizo dhidi ya Botswana na Burundi ni kipimo kizuri cha awali kwa kocha Salum Mayanga.
  Taifa Stars itamenyana na Botswana kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kucheza na Burundi Jumanne katika mechi za kirafiki za kimataifa.
  Hizo zitakuwa mechi za kwanza kabisa kwa kocha Mayanga, tangu achukue nafasi ya Charles Boniface Mkwasa aliyemaliza mkataba wake Januari.
  Na Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Mkude amesema mechi hizo zitakuwa kipimo kizuri cha awali kwa Mayanga katika kujenga timu imara ya kuingia nayo kwenye mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zinazohusisha wachezaji wanaocheza Ligi za nchini mwao pekee. 
  Jonas Mkude amesema kwamba mechi mbili mfululizo dhidi ya Botswana na Burundi ni kipimo kizuri cha awali kwa kocha Salum Mayanga

  “Mimi ninaona hizi mechi ni nzuri sana kwa kocha Mayanga baaada ya kuteua kikosi kwa mara ya kwanza ili kujua wachezaji aliowateua wakoje na pia kwa ujuma zitamsaidia katika kuanza kujenga kikosi imara cha kuwania tiketi ya AFCON na CHAN,”amesema Nahodha huyo wa Simba akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo. 
  Taifa Stars itaanza na Rwanda katika kuwania tiketi ya CHAN mwakani nchni Kenya na mechi ya kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kati ya Julai 14 na 16 kabla ya timu hizo kurudiana Uwanja wa Amahoro, Kigali kati ya Julai 21 na 23.
  Ikifanikiwa kuitoa Rwanda, Tanzania itamenyana na mshindi kati ya Uganda na ama Sudan Kusini au Somalia katika Raundi ya Tatu ya mchujo mechi ya kwanza ikichezwa kati ya Agosti 11, 12 na 13 na marudiano kati ya Agosti 18, 19 na 20, mwaka huu.
  Tanzania imewahi kushiriki mara moja tu fainali za CHAN, ambayo ilikuwa ni mwaka 2009 zikifanyika kwa mara ya kwanza kabia nchini Ivory Coast na kutolewa katika hatua ya makundi.
  Kwa upande wa AFCON, Taifa Stars imepangwa Kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho.
  Mshindi wa kila kundi atafuzu moja kwa moja AFCON ya 2019, wakati timu nyingine tatu zitakazomaliza nafasi ya pili na wastani mzuri zaidi ya nyingine zitafuzu kama washindi wa pili bora. 
  Tanzania imewahi kucheza mara moja tu fainali za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilitolewa hatua ya makundi pia. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MKUDE: MECHI HIZI ZITAMPA DIRA KOCHA MAYANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top