• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 25, 2017

  BANDA MCHEZAJI BORA WA FEBRUARI SIMBA SC

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  BEKI wa Simba, Abdi Banda ndiye mchezaji bora wa klabu hiyo kwa mwezi Februari mwaka huu, akiwa amewapiku winga Shiza Kichuya na mshambuliaji, Laudit Mavugo aliokuwa anachuana nao.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Sunday Manara amesema kwamba uteuzi umetokana na kura zilizopigwa na mashabiki wa klabu hiyo.
  “Tunapenda kuchukua fursa hii kumtangaza Abdi Banda kama mchezaji bora wa Februari, baada ya kura zilizopigwa na mashabiki. Banda amewazidi kwa kura Kichuya na Mavugo waliomfuatia,”amesema Manara.
  Abdi Banda (kulia) akiwa na kipa Mghana, Daniel Agyei (kushoto) ndiye mchezaji bora wa Simba wa mwezi Februari mwaka huu

  Pamoja na hayo, Manara amewataka wachezaji wa Simba kuendelea kujituma kuisaidia klabu hiyo kutimiza ndoto za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
  “Hizi tuzo ni kujenga hamasa kwa wachezaji wetu, lakini kitu kikubwa zaidi kwetu ni kuendelea kupigania ubingwa. Wachezaji waendelee kujituma ili kuisaidia timu kubeba ubingwa,”alisema Banda.
  Kwa upande wake, Banda ameshukuru kushinda tuzo hiyo na kuwashukuru mashabiki waliompigia kura baada ya kubaini mchango wake katika timu.
  “Nawashukuru benchi la Ufundi kwa kunipa nafasi, wachezaji wenzangu kwa ushirikiano wao kwangu na mashabiki walionipigia kura. Naahidi kuendelea kujituma kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu ili tutwae ubingwa wa Ligi Kuu,”amesema Banda. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BANDA MCHEZAJI BORA WA FEBRUARI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top