• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 23, 2017

  GSM YABORESHA MASLAHI YA WACHEZAJI MAJI MAJI ISISHUKE DARAJA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KAMPUNI ya GSM imesema kwamba imeboresha maslahi ya wachezaji wa Maji Maji FC ya Songea mkoani Ruvuma ili kuwahamasisha washinde mechi zote zilizosalia za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kuepuka kushuka Daraja.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana mjini Dar es Salaam, Mkuu wa Uwekezaji wa  GSM, ambao ni wafadhili wa Maji Maji, Hersi Said (pichani juu) amesema kwamba watahakikisha wanaibakiza Ligi Kuu timu hiyo.
  “Tumekwishafanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa, Chama cha Soka na wadau wakubwa wa Songea na wote wanataka Maji Maji inaki Ligi Kuu. Kwa hivyo tumeweka mkakati mzuri kuhakikisha tunashinda mechi zote timu ibaki Ligi Kuu,”alisema Hersi Said. 
  Katika kuhakikisha mpango unafanikiwa, uongozi wa Maji Maji umeanza kuwashughulikia wachezaji wativu wa nidhamu baada ya kuwasimamisha wanne, George Mpole, Peter Joseph, Yussuf Mfanyaje na Ibrahim Tende mapema wiki hii.
  Mwenyekiti wa Wana Lizombe hao, Humphrey Milanzi alisema kwamba wachezaji hao wamefanya utovu wa nidhamu ambao klabu haiwezi kuuvumilia na ili liwe fundisho kwa wachezaji wengine, uongozi umeamua kuwasimamisha.
  Aidha, Milanzi alisema kwamba kwa sasa uongozi unajikita katika jitihada za kuhakikisha unainusuru timu kushuka Daraja kwa kuhakikisha timu inashinda mechi zake zote saba zilizosalia za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.  
  Maji Maji kwa sasa inashika nafasi ya pili kutoka mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi 24, juu ya JKT Ruvu inayoshika mkia kwa pointi zake 20 za mechi 24 pia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: GSM YABORESHA MASLAHI YA WACHEZAJI MAJI MAJI ISISHUKE DARAJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top