• HABARI MPYA

    Sunday, March 26, 2017

    TUNAWATUMIAJE WATU KAMA YUSSUF BAKHRESA?

    MWEZI ujao itakuwa ni miaka nane kamili tangu mchezaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa afanye majaribio klabu ya West Ham United ya England.
    Akiwa mchezaji chipukizi wa klabu ya Yanga na taifa kwa ujumla, Ngassa alipatiwa nafasi ya majaribio ya West Ham Aprili mwaka 2009.
    West Ham ilikuwa inacheza Ligi Kuu ya England wakati huo chini ya kocha Mtaliano, Gianfranco Zola na Ngassa hakuonyesha woga.
    Alifanya vizuri majaribio yake na hata akamvutia kocha Zola, lakini kitu kimoja tu kikamkwamisha Mrisho.
    Mwili wake ‘mteke mteke’ ulimnyima nafasi ya kucheza Ulaya mapema na bahati mbaya anaelekea kumaliza soka yake bila kucheza barani humo kabisa, kinyume na matarajio ya wengi.
    Aliyefanikisha mipango ya Ngassa kwenda majaribio klabu ya Ligi Kuu England ni Yussuf Bakhresa, mtoto wa bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa.
    Yussuf Bakhresa ni mpenzi wa mpira wa siku nyingi tangu anasoma shule ya msingi na alipokuwa anasoma sekondari tu alikwishaanza kuwasaidia vijana wenzake kwenda kucheza soka Ulaya.
    Kali Ongala, Athumani Machuppa ni miongoni mwa watu waliosaidiwa mno na Yussuf Bakhresa hadi wakacheza Ulaya.
    Yussuf ameendelea na jitihada zake za kuwasaidia wachezaji wa Tanzania kupata timu Ulaya miaka yote, ingawa amekuwa akiyafanya hayo kimya kimya.
    Lakini Aprili mwaka jana tena Yussuf Bakhresa akaibuka katika mpango wa kumtafutia timu ya kuchezea Ulaya chipukizi wa Tanzania, Farid Mussa.
    Mipango ya awali ilikuwa Farid apelekwe timu ya La Liga, lakini baada ya kushauriwa na wenyeji wao, wakampeleka klabu ya Daraja la Kwanza, CD Teneriffe.
    Farid alitua Hispania kwa mara ya kwanza Aprili 21, mwaka jana baada ya kuichezea Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance mjini Tunis, Tunisia ikifungwa 3-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.
    Na ilimchukua wiki moja tu Farid kuwakuna kwa kipaji chake makocha wa Tenerife na kutaka kumnunua, lakini Azam ikakataa na kuamua kumtoa kwa mkopo Desemba, 2016.
    Na baada ya kutua Tenerife akaanza kuchezea kikosi cha U23 ili kupata uzoefu kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza kinachocheza Ligi Daraja la Kwanza nchini humo, maarufu kama Segunda.  
    Farid wiki hii amerejea nyumbani kwa mara ya kwanza tangu aondoke Desemba kwa ajili ya kuichezea timu ya taifa, Taifa Stars.
    Na jana akaungana na Nahodha, Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji kucheza kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichoifunga Botswana 2-0 katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Watanzania wakamuona Farid Mussa mpya na si yule wa mbio mbio tu wa Azam, bali anayecheza kwa nafasi, kwa kasi na asiyekaa na mpira muda mrefu.
    Namna alivyomtengenzea nafasi Samatta iliyozaa bao la pili ni tofauti kubwa na wachezaji waliobobea katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na chipukizi wa Ulaya.
    Unaona kabisa tunahitaji wachezaji wengi kwenda kuendeleza ujuzi wao Ulaya kama kweli tunataka kuinua soka yetu na si maneno matupu.
    Tunafanya vipi kuhakikisha tunakuwa na vijana wengi Ulaya?
    Yule Yussuf Bakhresa aliyempeleka Ngassa West Ham miaka nane iliyopita na akampeleka Farid Hispania mwaka jana ni mtu wa aina gani kwetu? Tunamtumiaje?
    Hayo ni maswali ambayo viongozi wetu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanapaswa kujiuliuza na kuchukua hatua kama lengo ni kutaka kuwa na timu nzuri ya taifa siku moja.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUNAWATUMIAJE WATU KAMA YUSSUF BAKHRESA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top