• HABARI MPYA

  Jumatano, Machi 29, 2017

  KICHUYA, MAVUGO, HAJIB WATUA BUKOBA KUIONGEZEA NGUVU SIMBA

  Na Mahmoud Zubeiry, BUKOBA
  NYOTA wa Burundi, Laudit Mavugo na wachezaji saba wa Simba waliokuwa na timu ya taifa ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wamewasili Bukoba leo asubuhi kuungana na wenzao kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumapili dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Wachezaji wa Tanzania ni mabeki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, viungo Said Ndemla, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin na mshambuliaji Ibrahim Hajib ambao walibaki Dar es Salaam kuichezea Taifa Stars dhidi ya Botswana Jumamosi ikishinda 2-0 na dhidi ya Burundi jana ikishinda 2-1.
  Nyota hao wanane tegemeo wa Wekundu wa Msimbazi wametua Bukoba kutekeleza wajibu wao kwa mwajiri wao, Simba SC ambaye atakuwa na kibaruwa kigumu Jumapili mbele ya timu ya kocha Mecky Mexime.
  Shiza Kichuya (kushoto) baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Bukoba leo 
  Mbaraka Yussuf naye amerejea kwenye timu yake, Kagera Sugar

  Wamewasili wakiongozana na Makamu wa Rais wa Simba SC, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). 
  Wamewasili kwa ndege ya shirika la Tanzania, ATCL wakiwa na mshambuliaji tegemeo wa Kagera Sugar, Mbaraka Yussuf ambaye naye alikuwa Taifa Stars.
  Na Mbaraka Yussuf ndiye aliyefunga bao la ushindi jana Taifa Stars ikiichapa 2-1 Burundi, baada ya Simon Msuva kufunga la kwanza na Laudit Mavugo kuwasazishia wageni.
  Wakati huo huo: Beki wa kati wa Simba SC, Mzimbabwe Method Mwanjali amewataka wachezaji wenzake wa klabu hiyo kujibidiisha kushinda kila mechi ili watimize ndoto za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
  “Mimi bado ninaumwa, lakini napenda kuwataki kila heri wachezaji wenzangu waisaidie timu kushinda. Wajitume washinde kila mechi ili tuchukue ubingwa,”alisema Mwanjali Dar e Salaam jana mchana.
  Mwanjali hajaenda Bukoba kwa sababu anauguza goti aliloumia katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Prisons Februari 11, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ikishinda 3-0.
  Siku hiyo, Mwanjali aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC, alitolewa kwa machela siku hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Mwinyi Kazimoto dakika ya 62.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KICHUYA, MAVUGO, HAJIB WATUA BUKOBA KUIONGEZEA NGUVU SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top