• HABARI MPYA

    Monday, March 20, 2017

    MPINZANI MPYA WA YANGA AFRIKA KUJULIKANA KESHO CAIRO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MPINZANI wa Yanga katika mchujo wa kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika anatarajiwa kujulikana kesho katika droo itakayopangwa mchana mjini Cairo, Misri yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    Droo hiyo itahusisha timu zilizovuka hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho dhidi ya zilizotolewa kwenye hatua hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Timu zilizotolewa Ligi ya Mabingwa zitamenyana na zilizosonga mbele Kombe la Shirikisho katika mechi za nyumbani na ugenini kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu barani.
    Winga wa Yanga, Simon Msuva akimiliki mpira mbele ya mchezaji wa Zanaco Dar es Salaam wiki mbili zilizopita
    Mechi za kwanza zinatarajiwa kucheza wikiendi ya Aprili 7 hadi 9 na marudiano yanatarajiwa kuwa wikiendi ya Aprili 14 hadi 16, mwaka huu.
    Timu zilizovuka hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho ni MC Alger, JS Kabylie za Algeria, Recreativo do Libolo ya Angola, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, El Masry, Smouha ya Misri, MAS Fes, Ittihad Tangier za Morocco, Rayon Sports ya Rwanda, Hilal El Obeid ya Sudan, Mbabane Swallows ya Swaziland, Platinum Stars, Supersport United za Afrika Kusini, Club Africain, CS Sfaxien za Tunisia na Zesco United ya Zambia.
    Zilizotolewa Ligi ya Mabingwa ni RC Kadiogo ya Burkina Faso, AC Leopards ya Kongo, AS Tanda ya Ivory Coast, TP Mazembe ya DRC, Gambia Ports Authority ya Gambia, Horoya ya Guinea, CNaPS ya Madagascar, AS Port Louis ya Mauritius, FUS Rabat, Wydad Athletic Club ya Morocco, Ferroviario Beira ya Msumbiji, Rivers United, Rangers ya Nigeria, Bidvest ya Afrika Kusini, Yanga SC ya Tanzania ya KCCA ya Uganda.
    Yanga SC imengukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Zanacio Jumamosi jioni Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia.
    Matokeo hayo yanamaanisha Yanga inatolewa kwa mabao ya ugenini, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MPINZANI MPYA WA YANGA AFRIKA KUJULIKANA KESHO CAIRO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top