• HABARI MPYA

    Monday, March 27, 2017

    STARS NA BURUNDI KIINGILIO SH 3,000 KESHO TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIINGILIO cha chini katika mchezo wa kesho wa kirafiki wa kimataifa kati ya wenyeji, Tanzania dhidi ya Burundi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa Sh. 3,000.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba viingilio vingine ni Sh. 15,000 kwa VIP A, Sh 10,000 kwa VIP B na VIP C na mchezo huo utaanza Saa 10:30 jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Huu ni mchezo wa pili kwa Taifa Stars kucheza ndani ya wiki moja baada ya ule wa awali dhidi ya The Zebras ‘Pundamilia’ wa Botswana uliofanyika Uwanja huo wa Taifa, jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
    Katika mchezo huo wa Jumamosi, Taifa Stars ambayo kwa sasa inanolewa na Salum Mayanga akisaidiwa na Patrick Mwangata ambao ni makocha wapya wa kikosi hicho, walishinda kwa mabao 2-0.
    Tayari Intamba Murugamba wametua nchini tangu jana Jumapili saa 4.30 asubuhi na kufikia Hoteli ya De Mag iliyoko, Kinondoni, Dar es Salaam na jioni yake walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini. Leo Jumatatu, inafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ndani ya kikosi hicho wamo washambuliaji wawili wanaotamba katika klabu za Simba na Young African za Dar es Salaam. Nyota hao ni Amisi Tambwe wa Young Africans na Laudit Mavugo wa Simba.
    Leo Jumatatu Machi 27, 2017 saa 8.30 alasiri nyota hao wakiongozana na kocha wao watazungumza na wanahabari namna walivyoajiandaa kucheza na Taifa Stars ambayo pia ina nyota wengi wanaocheza na wachezaji hao wa Burundi katika klabu za Simba na Young Africans.
    Wakati Mavugo ni mshambuluaji, anatarajiwa kuwa na wakati mgumu mbele ya walinzi mahiri ambao pia wako Simba kama vile Abdi Banda na Mohammed Hussein wakati Andrew Vicent anayetoka Young African atakuwa kisiki kwa Tambwe wanayecheza naye timu moja kama makocha watawapanga.
    Kwa upande wake, Mayanga alifurahishwa na ushindi wa Jumamosi iliyopita dhidi ya The Zebras ya Botswana na hivyo amehimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kesho.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS NA BURUNDI KIINGILIO SH 3,000 KESHO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top