• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 28, 2017

  ‘DOGO’ WA KAGERA, MBARAKA YUSSUF AIBEBA STARS

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI chipukizi, Mbaraka Yussuf Abeid ameanza vyema soka ya kimataifa baada ya kutokea benchi na kuifungia bao la ushindi Tanzania ikiilaza 2-1 Burundi katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mchezaji huyo wa Kagera Sugar ya Bukoba, alifunga bao hilo dakika ya 77 baada ya kupokea pasi ya Simon Msuva mbele kidogo ya mstari unaogawa Uwanja na kujivuta hadi ndani ya boksi kabla ya kufumua shuti lililogonga mwamba na kurudi, akauwahi na kufunga bao zuri.
  Mchezaji huyo aliyeibukia kikosi cha pili cha Simba, leo alikuwa anchezea mechi ya kwanza Taifa Stars baada ya kuitwa na kocha Salum Mayanga wiki iliyopita, lakini akacheza vizuri.
  Mbaraka Yussuf ametokea benchi na kuifungia bao la ushindi Taifa Stars ikiilaza 2-1 Burundi leo

  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa mwenye beji ya FIFA, Israel Mujuni Nkongo, hadi mapumziko Tanzania walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simon Happygod Msuva dakika ya 22 kwa shuti kali baada ya kuuwahi mpira uliopigwa kichwa na mshambuliaji Ibrahim Hajib kufuatia krosi ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyepasiwa na Farid Mussa.
  Baada ya bao hilo, Taifa Stars ikiongozwa na kiungo wa Tenerife ya Daraja la Kwanza Hispania, Farid Mussa iliendelea kupeleka mashambulizi langoni mwa Burundi, lakini ngome ya wageni ilikuwa imara.
  Kipindi cha pili, mshambuliaji Laudit Mavugo akatumia makosa ya mchezaji mwenzake wa Simba, beki Abdi Banda kuifungia bao la kusawazisha Burundi.
  Mshambuliaji wa Burundi, Laudit Mavugo akiwa amemdondokea beki wa Tanzania, Salim Mbonde
  Winga wa Tanzania Farid Mussa akimuacha chini beki wa Burundi, Gael Duhayindavya 
  Kiungo wa Tanzania, Himid Mao akimtoka Laudit Mavugo
  Mshambuliaji wa Tanzania, Ibrahim Hajib akimpita Djuma Nzeyimana
  Winga wa Tanzania, Simon Msuva akiruka juu dhidi ya mabeki wa Burundi kupiga kichwa

  Mavugo aliutokea mpira uliompita Banda na kwenda kumtungua kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’ dakika ya 53.
  Pamoja na Burundi kusaka bao la pili kwa juhudi, lakini walijikuta wakifungwa wao na kulala 2-1.
  Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Tanzania ndani ya siku tatu, baada ya Jumamosi kuifunga Botswana 2-0, mabao yote akifunga Nahodha Mbwana Samatta, ambaye hakucheza leo kufuatia kuondoka jana kurejea Ubelgiji kujiunga na klabu yake, KRC Genk.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Salim Mbonde, Himid Mao, Muzamil Yassin/Jonas Mkude, Salum Abubakr ‘Sure Boy’/Said Ndemla, Ibrahim Hajib/Shiza Kichuya, Farid Mussa/Mbaraka Yussuf na Simon Msuva.
  Burundi; Jonathan Nahimana, Gael Duhayindavya, Rashid Harerimana, Omary Moussa, David Nshirimimana/Eric Ndoyirobija, Youssouf Ndayishimiye, Tresor Ndikumana, Jean Ndarusanze/Franck Barirengako, Laudit Mavugo, Kiza Fataki/Moustapha Selemani na Djuma Nzeyimana/Sudi Ntirwaza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ‘DOGO’ WA KAGERA, MBARAKA YUSSUF AIBEBA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top