• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 26, 2017

  WAZIRI MPYA WA MICHEZO AWAAMBIA TFF; "FUTENI UTAMADUNI WA KUFUNGWA FUNGWA"

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAZIRI mpya wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amewaambia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wahakikishe wanafuta utamaduni wa timu za Tanzania kufungwa. 
  "Watanzania tumechoka na huu uteja, kusukumwa sukumwa tu kwenye soka. Ni hamu ya watanzania sasa tuonekane katika ulimwengu wa soka", alisema jana Waziri Dk. Mwakyembe aliyezungumza na Kamati ya Hamasa kwa Serengeti Boys alipokutana nayo kwa mara ya kwanza jana Machi 25, mwaka huu.
  Waziri alikwenda mbali kwa kuiagiza Wizara yake yote ijikite kuhakikisha maandalizi ya Serengeti Boys yanakamilika kwa wakati. 
  Dk. Harrison Mwakyembe amewaambia TFF wahakikishe wanafuta utamaduni wa timu za Tanzania kufungwa

  "Nataka Wizara yangu yote sasa wimbo wetu uwe Serengeti Boys," amesema Dk. Mwakyembe.
  Katika hafla hiyo, Dk Mwakyembe amempongeza mtangulizi wake, Mheshimiwa Nape Nnauye kwa kuunda Kamati ya Serengeti Boys ili kutoa hamasa ya Watanzania kwa timu yao. 
  Alisema Serengeti Boys ni nyota wanaoinukia (upcoming stars) na wanampa sababu ya kuanza kwenda mpirani tena. 
  Waziri Dk Mwakyembe aliendelea kusema kuwa michezo ya leo inahitaji uwekezaji hivyo Wizara yake itahakikisha kuwa jukumu hilo analibeba.
  "Naona kama imechelewa, lakini bado muda upo, tukimbie, nataka Wizara nzima wimbo wetu uwe Serengeti Boys", alisema kwa hamasa kubwa. 
  Dk Mwakyembe amempongeza Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Mwenyekiti wa Kamati ya Serengeti Boys, Charles Hilary kwa mafanikio ya program ya mageuzi ya soka nchini. 
  Naye Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yussuf Singo alisema sasa imechoka kuwa kichwa cha mwenda wazimu na hivyo Taifa limeazimia kucheza Kombe la Dunia kupitia vijana wa Serengeti Boys. 
  Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema kufuzu kwa Serengeti Boys kucheza fainali za AFCON ni sifa pekee na mwanzo mpya wa mageuzi makubwa ya soka la Tanzania.
  Amesema maandalizi ya ushiriki wa fainali za AFCON zitahitaji takriban Shilingi bilioni moja. 
  Amesema mikakati mbalimbali imeandaliwa kuchangisha kiasi hicho cha fedha, ikiwa ni pamoja na kuandaa chakula cha hisani. 
  Waziri Mwakyembe amesema atahakikisha fedha hiyo inapatikana ili vijana wa Serengeti Boys waweze kufuzu kucheza kombe la dunia huko India mwishoni mwa mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WAZIRI MPYA WA MICHEZO AWAAMBIA TFF; "FUTENI UTAMADUNI WA KUFUNGWA FUNGWA" Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top