• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 24, 2017

  ULIMWENGU AWASIKITIKIA MAZEMBE, ASEMA KUBADILI MAKOCHA KUNAWAPONZA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesema klabu yake ya zamani, TP Mazembe ya DRC inaathiriwa na kubadili makocha mara kwa mara.
  Kwa msimu wa pili mfululizo, Mazembe imetolewa katika Ligi ya Mabingwa ya Afrika na kuangukia Kombe la Shirikisho na Ulimwengu anayechezea AFC Eskilstuna ya Sweden kwa sasa amesema timu hiyo inahitaji kutulia na mwalimu mmoja. 
  “Muda mwingine kubadilisha sana makocha inakuwa inaleta ugumu, maana kila kocha anakuja na mtindo wake wa ufundishaji, hivyo wachezaji inawawia vigumu kuanza mfumo kuuzoea mfumo mwingine,”amesema Ulimwengu akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana kwa simu kutoka Sweden.
  Thomas Ulimwengu amesema kubadili makocha mara kwa mara kunaiponza klabu yake ya zamani, TP Mazembe ya DRC  

  Pamoja na hayo, Ulimwengu amesema anaamini Mazembe bado ni timu nzuri na inaweza kutetea Kombe la Shirikisho Afrika. 
  Mapema wiki hii, Mazembe iliachana na kocha Mfaransa, Thierry Froger baada ya kutolewa katika hatua hatya ya 32 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika na CAPS United ya Zimbabwe kwa mabao ya ugenini, ikitoa sare ya 1-1 Lubumbashi na 0-0 Harare.
  Mazembe imeangukia katika kapu la kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na itamenyana na JS Kabylie ya Algeria baada ya droo iliyopangwa leo mjini Cairo, Misri. 
  Mechi za kwanza zinatarajiwa kucheza wikiendi ya Aprili 7 hadi 9 na marudiano yanatarajiwa kuwa wikiendi ya Aprili 14 hadi 16, mwaka huu.
  Froger alijiunga na Mazembe Februari 15, siku chache kabla ya kumenyana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mechi ya Super Cup ya CAF, akichukua nafasi ya Mfaransa mwenzake, Hubert Velud aliyeondoka mwishoni mwa mwaka jana kuhamia Etoile du Sahel ya Tunisia.
  Wasiwasi juu ya mustakabali wa Froger ulianza mapema tu baada ya kushindwa kuwawezesha mabingwa hao wa Kombe la Shirikisho kubeba Super Cup ya CAF kufuatia kufungwa 1-0 na Mamelodi Februaeri 18, mwaka huu Uwanja wa Lucas Masterpieces Moripe mjini Pretoria, Afrika Kusini.
  Ulimwengu kwa sasa anachezea AFC Eskilstuna baada ya kung'ara TP Mazembe  

  Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi 2011 TP Mazembe alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
  Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
  Ulimwengu anajivunia kushinda mataji makubwa akiwa na Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia kabla ya kuhamia Ulaya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ULIMWENGU AWASIKITIKIA MAZEMBE, ASEMA KUBADILI MAKOCHA KUNAWAPONZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top