• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 31, 2017

  KABURU ASEMA SIMBA HAITAICHUKULIA POA KAGERA SUGAR JUMAPILI

  Na Mahmoud Zubeiry, BUKOBA
  MAKAMU wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema kwamba hawataidharau Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bali wataingia kwa nguvu zao zote kuhakikisha wanashinda.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana mjini hapa, Kaburu alisema kwamba katika hatua kama hizi wanapaswa kuwa makini ili kutimiza ndoto za kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu.
  Kaburu alisema wakiteleza kidogo wanaweza kujikuta wanawapa nafasi mahasimu wao, Yanga SC wanaowafuatia kwa karibu kwenye mbio za ubingwa.
  Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ (kushoto) amesema kwamba hawataidharau Kagera Sugar Jumapili 

  “Kitu ambacho tumekuwa tukiwaambia wachezaji wetu mara kwa mara ni kutodharaua mechi. Na katika kuelekea mchezo huu na Kagera, tunawakumbusha san asana kutodharau mechi,”alisema Kaburu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Kaburu amesema anaiamini timu yake ni nzuri kwa sasa na ina uwezo wa kuifunga timu yoyote ya Ligi Kuu, lakini mambo yanaweza kuwa tofauti iwapo wataingiza dharau kazini.
  Simba inatarajiwa kuwa mgeni wa Kagera Sugar keshokutwa katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Kaitaba Bukoba.
  Ni mchezaji mmoja tu wa Simba atakosekana katika mchezo huo, beki Method Mwanjali anayesumbuliwa na maumivu – lakini zaidi ya hapo Wekundu wa Msimbazi wametua Bukoba na jeshi lao kamili.
  Ikumbukwe Simba ndiyo wanaongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 55 dhidi ya 53 za mabingwa watetezi, Yanga SC baada ya kila timu kucheza mechi 24.
  Wakati Simba wakiwa Uwanja wa Kaitaba kusaka pointi zaidi Jumapili, mahasimu wao, Yanga Jumamosi watashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Azam FC.
  Azam FC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zao 44, ikifuatiwa na Kagera Sugar yenye pointi 42 baada ya timu zote kucheza mechi 24 pia.
  Kwa ujumla, Ligi Kuu inaendelea wikiendi hii baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha mechi za michuanao ya klabu Afrika na za kimataifa – mbali na Simba kuwa wageni wa Kagera mjini Bukoba na Yanga kuonyeshana kazi na Azam Dar es Salaam, nyasi za viwanja vingine vitano zitawaka moto.
  Uwanja wa Sokoine Mjini Mbeya, Mbeya City Wataikaribisha, Ruvu Shooting, wakati  
  Jumapili African Lyon wataikaribisha Stand United Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Prisons wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine Mbeya, Mwadui FC wataikaribisha JKT Ruvu Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Maji Maji FC wataikaribisha Toto African Uwanja wa Maji Maji Songea.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KABURU ASEMA SIMBA HAITAICHUKULIA POA KAGERA SUGAR JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top