• HABARI MPYA

    Thursday, March 30, 2017

    NYASI BANDIA ZA SIMBA ZAPIGWA MNADA WAMESHINDWA KUZILIPIA USHURU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NYASI bandia za Simba ziko hatarini kupigwa mnada, baada ya klabu hiyo kushindwa kuzilipia ushuru tangu ziwasili Oktoba mwaka jana.
    Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema leo kwamba wana taarifa za mpango wa kupigwa mnada nyasi hizo na wapo kwenye mchakato wa kuzikomboa.
    “Ni kweli kwa kawaida Bandarini kuna utaratibu, mzigo unapofika lazima ulipiwe utoke, ikishindikana hivyo unapigwa mnada. Kwa hiyo lazima tujitahidi tuzikomboe,”alisema.
    Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Ujenzi wa Uwanja Bunju Complex wa klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba anashangaa kusikizia nyasi hizo bado hazijalipiwa, wakati fedha zilikwishapatikana.
    “Unaponiambia hivyo ninashangaa, kwa sababu tulikwishafanya mpango fedha zikapatikana za kulipia hizo nyasi, sasa kuambiwa hazijalipiwa hadi sasa sijui ni kwa nini,”alisema Hans Poppe na kuongeza; “Ngoja niwasiliane na wenzangu, mimi nipo Kenya kwa sasa,”alisema. 
    Mbali na Hans Poppe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Wajumbe wengine wa Kamati ya Bunju Complex ni Salim Muhene, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji kuwa Makamu wa Mwenyekiti.
    Katibu ni Issa Batenga wakati Wajumbe wa Kamati hiyo ni Ally Suru, ambaye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Adam Mgoyi ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Wadhamini, Crescentius Magori, Imani Kajula na Jerry Yambi.
    Taarifa zaidi zinasema kampuni ya udalali na minada ya Majembe inaanza kuzipiga mnada nyasi hizo leo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NYASI BANDIA ZA SIMBA ZAPIGWA MNADA WAMESHINDWA KUZILIPIA USHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top