• HABARI MPYA

  Jumapili, Agosti 25, 2013

  AZAM FC WAINGIA TABORA USIKU USIKU TAYARI KUWAVAA KIBOKO YA SIMBA RHINO JUMATANO

  Na Mahmoud Zubeiry, Tabora IMEWEKWA AGOSTI 25, 2013 SAA 5:36 USIKU
  KIKOSI cha Azam FC kimewasili usiku huu mjini Tabora, kikitokea Morogoro tayari kwa mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumatano dhidi ya wenyeji, Rhino Rangers Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini hapa.
  Azam imefika majira ya saa 4:30 tangu iondoke asubuhi mjini Morogoro na imefikia katika hoteli ya Mwafrika, jirani kabisa na Uwanja wa Mwinyi. 
  Meneja wa Azam FC, Jemadari Said Kazumari amesema timu itapumzika kutwa ya kesho na jioni itafanya mazoezi, kujiandaa na mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na wakazi wa mjini hapa.
  Wako Mboka Manyema; Wachezaji wa Azam kulia John Bocco, Erasto Nyoni katikati na kushoto Said Mourad

  Azam ilianza Ligi Kuu kwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar jana kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
  Mtibwa walitangulia kupata bao kupitia kwa Juma Luizio dakika ya nne kabla ya Aggrey Morris kuisawazishia Azam kwa penalti dakika ya 19. 
  Baada ya mechi hiyo, Azam inayofundishwa na kocha Muingereza, Stewart Hall ilikwenda kulala mjini Morogoro na asubuhi wakaondoka na basi lao kubwa la kisasa kuja Tabora, walipofika usiku huu.
  Rhino, inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, nayo ilianza Ligi Kuu kwa sare ya kufungana 2-2 na Simba SC jana Mwinyi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: AZAM FC WAINGIA TABORA USIKU USIKU TAYARI KUWAVAA KIBOKO YA SIMBA RHINO JUMATANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top