• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 27, 2013

  ABBEL DHAIRA AMEFUNGWA MABAO 18 KATIKA MECHI 11 ALIZODAKA SIMBA SC HADI SASA, NI MECHI MOJA TU ALIMALIZA BILA KUFUNGWA TENA DHIDI YA KAHAMA UNITED

  Na Mahmoud Zubeiry, Tabora, IMEWEKWA AGOSTI 27, 2013 SAA 6:58 MCHANA
  KIPA Mganda wa Simba SC, Abbel Dhaira amekwishafungwa mabao 18 katika mechi 11 alizoidakia klabu hiyo tangu Januari mwaka huu alipojiunga nayo, akitokea IBV ya Ligi Kuu ya Iceland, huo ukiwa ni wastani wa karibu mabao mawili kila mechi.
  Na mabao mengi aliyofungwa Dhaira yanatokana na mipira ya chini, lakini imeonekana wazi kutokana na urefu wake ni vigumu kumfunga kwa mipira ya juu kipa huyo.
  Jumamosi kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora, Dhaira alifungwa mara mbili kwa mipira ya chini, yote ikiwa mipira ya adhabu wakati Simba SC ikitoka sare ya 2-2 na Rhino Rangers katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Mabao 18, mechi 11; Abbel Dhaira amekuwa na mwanzo mbaya Simba SC

  Hata kocha Mkuu wa Simba SC, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ alisikitishwa na kipa huyo Mganda akisema Abbel Dhaira amewaangusha kwa kufungwa mabao rahisi.
  Mechi ya kwanza Dhaira kuidakia Simba SC ilikuwa ni dhidi ya Bandari Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu, ambako alifungwa bao moja, timu hiyo ikitoa sare ya 1-1.
  REKODI YA DHAIRA SIMBA SC:
  Simba SC 1-1 Bandari (Kombe la Mapinduzi, alifungwa moja)
  Simba SC 0-1 U23 Oman (Kirafiki, alifungwa moja)
  Simba SC 1-3 Qaboos (Kirafiki, alidaka nusu akafungwa mawili)
  Simba SC 0-4 R. de Libolo (Ligi ya Mabingwa, alifungwa manne) 
  Simba SC 2-1 Coastal Union (Ligi Kuu, alifungwa moja)
  Simba SC 2-2 Azam FC  (Ligi Kuu, alifungwa mbili)
  Simba SC 1-0 Kahama United (Kirafiki, Kahama hakufungwa)
  Simba SC 1-2 URA  (Kirafiki, Taifa, alifungwa mbili)
  Simba SC 0-1 Coastal (Kirafiki, Tanga alifungwa moja)
  Simba SC 4-1 SC Villa (Simba Day, Taifa alifungwa moja)
  Simba SC 2-2 Rhino (Ligi Kuu, alifungwa mbili)
  Baada ya hapo, akaidakia Simba ikicheza dhidi ya U23 ya Oman, ambako alifungwa moja, timu hiyo ikifungwa 2-1 na akadaka dhidi ya timu ya Jeshi Oman na kufungwa mara mbili, timu hiyo ikilala 3-2. Bao lingine alifungwa Juma Kaseja, ambaye ametemwa msimu huu. 
  Akadaka tena katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Recreativo de Libolo ya Angola na kufungwa mabao manne, timu hiyo ikilala 4-0.
  Akarudi Dar es Salaam na kudaka katika mchezo wa Ligi Kuu msimu uliopita dhidi ya Coastal Union ya Tanga na kufungwa bao moja, timu hiyo ikishinda 2-1.
  Akadaka tena katika Ligi Kuu dhidi ya Azam na kafungwa mabao mawili, moja la penalti timu hizo zikitoka 2-2, huo ukiwa mchezo wake wa mwisho Simba SC msimu uliopita.
  Nini tatizo? Abbel Dhaira amepoteza uhodari wake ulioivutia Simba SC hadi ikamsajili

  Akarejea kwenye mechi za kujiandaa na msimu huu, akadaka dhidi ya Kahama United mkoani Shinyanga na kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na timu hiyo alifanikiwa kumaliza mechi bila kufungwa. Na huo ndio mchezo pekee ambao Dhaira alidaka bila kufungwa Simba SC.
  Akadaka tena dhidi ya URA ya kwao, Uganda katika mchezo wa kirafiki na kutunguliwa mara mbili timu hiyo ikilala 2-1 katika mchezo huo wa kirafiki, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Akaenda Tenga kwenye mchezo wa kirafiki na Coastal, akafungwa moja, Wekundu wa Msimbazi wakilala 1-0. 
  Akadaka tena dhidi ya SC Villa ya kwao, Uganda na kufungwa bao moja, timu hiyo ikishinda 4-1 kabla ya Jumamosi kufungwa mawili katika sare ya 2-2 na Rhino.
  Kwa kuwa kipa huyo ndiye chaguo la kwanza la Simba SC kwa sasa, bila shaka na kesho atasimama tena langoni katika mchezo dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha, kwani kipa wa pili Andrew Ntalla aliyesajiliwa kutoka Kagera Sugar msimu huu, bado hajaaminiwa sana.  
  Haaminiwi bado; Kipa Andrew Ntalla aliyesajiliwa kutoka Kagera Sugar haaminiwi sana 

  Hakuna shaka Dhaira ni kipa mzuri, lakini inaonekana wazi tangu ametua Simba SC kidogo kiwango chake kimeshuka- pamoja na ukweli kwamba Wekundu wa Msimbazi bado hawajapata safu imara ya ulinzi. 
  Kisoka, Dhaira aliibukia Express mwaka 2006 ambako alicheza hadi 2008 akahamia URA, alikocheza hadi 2010 akahamia AS Vita ya DRC ambayo ilimuuza IBV mwaka 2012 alikodaka mechi 30 bila kufungwa bao hata moja, hadi anahamia Simba mwaka huu.
  Amekuwa akiidakia timu ya taifa ya Uganda tangu mwaka 2009 na tangu 2011 amekuwa kipa namba moja wa timu hiyo, ingawa kwa sasa anakabiliwa na ushindani wa aliyekuwa kipa wa kwanza wa timu hiyo kabla yake, Dennis Onyango pamoja Muwonge Hassan anayeibukia vizuri.
  Dhaira alidaka mechi moja tu na kuumia katika Kombe la Challenge mwaka jana na baada ya hapo, Muwonge akadaka hadi kuipa timu ubingwa. Muwonge tena akaipa Uganda tiketi ya CHAN- na sasa anajitengenezea mazingira mazuri The Cranes mbele ya Onyango na Dhaira. 
  Mabao rahisi; Dhaira alifungwa mabao rahisi dhidi ya Rhino hadi Kibadeni akalalamika

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: ABBEL DHAIRA AMEFUNGWA MABAO 18 KATIKA MECHI 11 ALIZODAKA SIMBA SC HADI SASA, NI MECHI MOJA TU ALIMALIZA BILA KUFUNGWA TENA DHIDI YA KAHAMA UNITED Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top