• HABARI MPYA

  Ijumaa, Agosti 23, 2013

  YANGA WAANZA KUTETEA TAJI NYUMBANI KESHO LIGI KUU, SIMBA NA AZAM WAKO UGENINI

  Na Boniface Wambura, IMEWEKWA AOSTI 23, 2013 SAA 11:54 JIONI
  MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/2014 inaanza kutimua vumbi kesho (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja saba tofauti huku mabingwa watetezi Yanga wakianza kutetea ubingwa wao kwa kuikaribisha Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
  Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Azam ya Dar es Salaam na wenyeji Mtibwa Sugar. Oljoro JKT itaikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
  Yanga SC wanaanza kutetea taji na Ashanti kesho

  Mgambo Shooting itaoneshana kazi na JKT Ruvu ambayo hivi sasa iko chini ya Kocha Mbwana Makata. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Rhino Rangers itakwaruzana na Simba katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
  Mbeya City iliyopanda VPL msimu huu itapimana ubavu na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku Ruvu Shooting ikiialika Mabatini, Mlandizi timu ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya.
  Mzunguko wa pili wa ligi hiyo utachezwa Agosti 28 mwaka huu. Baada ya hapo ligi itasimama kupitisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Gambia na Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul. VPL itaingia mzunguko wa tatu Septemba 14 mwaka huu.
  Simba SC watakuwa Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora na Rhino FC

  Wakati huo huo: Tiketi za elektroniki zitaanza kutumika katika mzunguko wa nne wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) utakaoanza Septemba 18 mwaka huu. Tayari benki ya CRDB ambayo ndiyo ilishinda tenda hiyo imeshakamilisha ufungaji wa vifaa kwa ajili ya matumizi ya tiketi hizo katika viwanja vyote.
  Hivi sasa Serikali ambayo ndiyo inamiliki Uwanja wa Taifa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na CRDB zinashughulikia mfumo wa tiketi hizo kwenye uwanja huo ambao ndiyo ulikuwa haujakamilika kwa matumizi katika upande huo.
  Azam watakuwa Uwanja wa Manungu na Mtibwa Sugar 

  Mfumo (system) iliyoko kwenye uwanja huo inapishana na ule utakaotumiwa na CRDB, hivyo pande husika zinashughulikia suala hilo ili mifumo hiyo iweze kuingilia.
  Pia mashine za kuchapia (printer) kwa ajili ya tiketi ambazo CRDB wameziagiza kutoka nje ya nchi zinatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu.
  Hivi sasa CRDB inashughulikia ufungaji wa vifaa vya matumizi ya tiketi za elektroniki iwemo turnstiles kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambao mwanzoni hakuwemo kwenye mpango huo kutokana na Mkoa wa Tabora kutokuwa na timu ya Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA WAANZA KUTETEA TAJI NYUMBANI KESHO LIGI KUU, SIMBA NA AZAM WAKO UGENINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top