• HABARI MPYA

    Friday, August 30, 2013

    AZAM FC WATUA DAR USIKU HUU BAADA YA SAA 15 BARABARANI

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA AGOSTI 30, 2013 SAA 9:40 USIKU
    KIKOSI cha Azam FC, kimewasili salama usiku huu majira ya saa 6:45 usiku mjini Dar es Salaam baada ya safari ndefu ya saa 15 barabarani, kikitokea mkoani Tabora ambako jana kilimenyana na wenyeji, Rhino Rangers katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
    Azam imewasili na basi lake la kisasa aina ya Yutong, wachezaji wake wakiwa na furaha ya ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu, baada ya kuwalaza wenyeji 2-0.
    Azam imerejea Dar es Salaam kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba wiki mbili zijazo, ikiwa imevuna pointi nne tayari baada ya mechi mbili ngumu za ugenini, dhidi ya Mtibwa Sugar (1-1) na Rhino (2-0).
    Azam ndani ya basi lao

    Wachezaji wa Azam ambao hawajaitwa kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachoingia kambini asubuhi ya leo, watafanya mazoezi jioni ya leo, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na kupewa mapumziko ya siku mbili za wikiendi, kabla ya kuendelea na mazoezi Jumatatu.
    Wachezaji wa Azam walioitwa timu ya taifa inayojiandaa na mchezo wa mwisho wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Gambia Septemba 7 ni makipa Aishi Manula na Mwadini Ally, mabeki Erasto Nyoni na Aggrey Morris, viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya na Khamis Mcha ‘Vialli’ na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’.
    Hata hivyo, Sure na Bocco wamewasili wakiwa wagonjwa na wanataka kuomba ruhusa ya kuendelea na tiba.
    Kulia mfungaji wa bao la pili Seif Abdallah Karihe, kushoto Said Mourad


    John Bocco na Khamis Mcha kulia

    Mwadini Ally kulia na Karume kushoto

    Basi linawasili Dar es Salaam

    Katika mchezo wa Tabora, iliwachukua dakika 11 tu Azam baada ya kipindi cha pili kupata bao la kwanza lililofugnwa na Gaudence Mwaikimba, dakika ya 56, baada ya kupokea pasi ya kutanguliziwa pembeni kulia na Erasto Nyoni, kisha akamtoka beki wa Rhino, Hussein Msabila na kuingia ndani kidogo na kipa Abdulkarim Mtumwa akavutika, hivyo kumpa kazi rahisi mshambuliaji wa Azam kukwamisha mpira nyavuni.    
    Seif aliyeingia kipindi cha pili, alifunga bao la pili dakika ya 78 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa, kufuatia mpira wa adhabu wa Jabir Aziz. 
    Mchezo ulikuwa mkali na wa nguvu jambo ambalo lilimfanya mfungaji bora wa Ligi Kuu, Kipre Tchetche acheze kwa dakika 28 tu baada ya kuumia mguu wa kulia kufuatia kukanyagwa na beki wa Rhino, Laban Kambole. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AZAM FC WATUA DAR USIKU HUU BAADA YA SAA 15 BARABARANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top