• HABARI MPYA

    Monday, August 26, 2013

    KUINGIA BURE MPIRANI NI KUZITIA UMASIKINI KLABU ZETU

    IMEWEKWA AGOSTI 26, 2013 SAA 2:10 ASUBUHI
    WAKATI zikiwa zimebaki siku kumi kabla kuanza kwa ligi kuu ya soka ya Zanzibar Grand Malt, ni vyema nitoe tahadhari kwa mashabiki wanaopenda kuingia viwanjani bure.
    Tayari Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kimeshatangaza kwamba ligi hiyo itaanza Septemba 5, mwaka huu katika viwanja vya Mao Tse Tung Unguja na Gombani Pemba.
    Limekuwa jambo la kawaida kwa wapenzi wengi wa mpira wa miguu hapa nchini kulazimisha waachiwe waingie viwanjani bila kununua tiketi kwa madai kwamba wao ni miongoni mwa wanachama wa klabu zinazocheza au wadau muhimu wa soka.

    Mbali na hao, pia mara nyingi tumekuwa tukishuhudia watu wazito ambao ni viongozi wanaoshika nyadhifa mbalimbali serikalini wakitumia nafasi zao hizo kutaka waingie bure kutazama mechi za mpira wa miguu. 
    Katika hali ya kawaida, isingetarajiwa watu kama hao ambao wanapata mishahara mikubwa na marupurupu manono, washindwe kununua tiketi na kung’ang’ania dezo.
    Kama inavyofahamika, timu zetu Zanzibar ni masikini na zinajiendesha katika mazingira magumu, hivyo unapofika msimu wa ligi hutarajia angalau kuingiza vijisenti vichache vitakavyowawezesha kugharamia mahitaji ya wachezaji.
    Pamoja na kwamba ligi kuu inaendelea na udhamini wa kinywaji cha Grand Malt kwa mwaka wa pili sasa, lakini sote tunajua kuwa udhamini huo si mkubwa kiasi cha kuzifanya timu zimalize msimu bila ya kuwa na madeni.
    Tushukuru kuwa angalau Grand Malt imekubali kuibeba ligi kuu japo kwa hizo shilingi milioni 140 kwa msimu mmoja, lakini ieleweke kuwa kiasi hicho ni ujazo wa kiganjani tu na kamwe hazizifikishi timu popote zaidi ya kupata nauli ya kusafiri kati ya Unguja na Pemba.
    Kwa hivyo, si busara kwa sisi tunaotaka kwenda viwanjani kushuhudia mechi za ligi hiyo kufumbia macho jambo hilo na kutumia vyeo na ulwa tulionao kuhalalisha kuingia bure.
    Kama wewe ni Katibu Mkuu wa wizara fulani, Mkurugenzi, Meneja, Waziri au Naibu Waziri, unashindwaje kutoa shilingi 2000 au 5000 kukata tiketi ya mpirani na kulazimisha uachiwe upite bure? 
    Hebu wafikirie wachezaji unaokwenda kuwatazama kwamba nao wako kazini na wanatarajia ujira kwa shughuli hiyo.
    Kama wewe unavyotegemea maslahi kutokana na ajira yako, basi elewa kwamba na vijana hao pia wanataka malipo ya jasho lao ambalo ni hizo tiketi zinazouzwa viwanjani.
    Waswahili husema; “Starehe gharama”, hivyo kama kweli unataka kuburudika, usiwe na mkono wa buli na kuziona fedha zako kuwa ni tamu kuliko starehe unayoifuata viwanjani. 
    Tununue tiketi ili tuzisaidie timu zetu kwani nazo zinafanya kazi ya kutuburudisha na hivyo zinahitaji kulipwa.
    Katika hili, ZFA inapaswa kuiga mfano wa wenzao wa TFF waliotangaza wazi kwamba hakuna cha bure katika mechi inazoziandaa, na watu wote ukitoa watu wa vyombo vya habari na walinzi, wanapaswa kulipa. 
    ZFA ianzishe kanuni kupima afya za wachezaji wanaosajiliwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KUINGIA BURE MPIRANI NI KUZITIA UMASIKINI KLABU ZETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top