• HABARI MPYA

    Tuesday, August 27, 2013

    BILA ANGALAU ‘BUKU TANO’, HUZIONI YANGA NA COASTAL KESHO TAIFA

    Na Boniface Wambura, IMEWEKWA AGOSTI 27, 2013 SAA 9:30 ALASIRI
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaingia katika Raundi ya pili kesho (Agosti 24 mwaka huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani huku macho na masikio ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Yanga na Coastal Union.
    Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna atakuwa Omari Walii kutoka Arusha.
    Mtibwa Sugar itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wakati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora utakuwa mwenyeji wa pambano kati ya wenyeji Rhino Rangers na Azam.
    Yanga SC watacheza na Coastal Taifa kesho 

    Vumbi lingine litatimka kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati maafande wa JKT Ruvu watakapokwaruzana na wenzao wa Tanzania Prisons kutoka Mbeya. Mbeya City na Ruvu Shooting zitacheza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
    Jiji la Tanga litakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ashanti United itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Oljoro JKT itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
    Coastal Union imepania kuipokonya Yanga SC ubingwa msimu huu 

    Wakati huo huo: Ratiba ya michuano ya U15 Copa Coca-Cola ngazi ya kanda mwaka huu itapangwa keshokutwa (Agosti 29 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
    Michuano hiyo ya kanda itaanza Septemba Mosi mwaka huu wakati mikoa inakumbushwa kuwa inatakiwa iwe imewasilisha usajili wa wachezaji wao kufikia Agosti 28 mwaka huu kupitia email ya TFF ambayo ni tanfootball@tff.or.tz na nakala kwa madadi_salum@ yahoo.com
    Pia mikoa inakumbushwa kutowajumuisha wanafunzi wa darasa la saba katika timu zao katika ngazi ya kanda na fainali itakayochezwa Dar es Salaam kuanzia Septemba 7 mwaka huu kwa vile watakuwa katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi. Timu zinatakiwa kufika vituoni Agosti 30 mwaka huu.
    Kanda hizo ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Singida inaunda Kanda ya Arusha.
    Zanzibar itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja wakati Kanda ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara, Temeke na mkoa mmoja wa Unguja.
    Kanda ya Mbeya inaundwa na Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma wakati Dodoma, Morogoro, Pwani na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.
    Mwanza itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za Arusha timu mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro itaingiza timu mbili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BILA ANGALAU ‘BUKU TANO’, HUZIONI YANGA NA COASTAL KESHO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top