• HABARI MPYA

  Jumamosi, Agosti 24, 2013

  RAGE APAA USIKU HUU KWENDA BUJUMBURA KUFUATA ITC ZA WACHEZAJI WARUNDI WA SIMBA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, Tabora IMEWEKWA AGOSTI 24, 2013 SAA 2:48 USIKU
  MWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage ameondoka leo usiku Dar es Salaam kwenda Bujumbura, Burundi kufuatilia Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) za wachezaji wake wawili, beki Kaze Gilbert na mshambuliaji Tambwe Amisi.
  Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ ameiambia BIN ZUBEIRY mjini hapa leo kwamba, Rage amelazimika kwenda Burundi baada ya kuona ITC hizo zinachelewa.
  Chabo kwa dirishani; Amisi Tambwe akiangalia mchezo wa leo akiwa ndani ya basi la Simba SC Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi

  Rage anapambana ili wachezaji hao waweze kucheza mechi ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha Jumatano, baada ya leo kukwama kucheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya wenyeji, Rhino Rangers mjini hapa.  
  Wachezaji hao waliosajiliwa kutoka mabingwa wapya wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Vital’O ya kwao, leo walikuwapo Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi kuishuhudia timu yao ikilazimishwa sare ya 2-2 na Rhino.
  Kocha Mkuu wa Simba SC, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ amesema kukosekana kwa wachezaji hao leo kumechangia matokeo ya sare kwa timu yake.
  Nawafuata huko huko tukamalizane; Aden Rage ameenda Burundi kufuata ITC za wachezaji

  Kibadeni, ambaye pia alisema kipa Mganda Abbel Dhaira amewaangusha leo kwa kufungwa mabao rahisi, alisema aliwaandaa wachezaji hao kwa ajili ya kucheza leo, hivyo kuwakosa imemvurugia mipango yake.
  “Nilitegemea sana kuwatumia wale mabwana leo, lakini kwa bahati mbaya, ITC zao zimechelewa kufika na tumeshindwa kuwatumia, kwa kweli imeniangusha sana,”alisema.
  Simba SC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo. 
  Mabao yote ya Simba SC yalifungwa na kiungo Jonas Mkude dakika za 10 na 38 kwa penalti, wakati ya Rhino yalifungwa na Iman Noel dakika 36 na Saad Kipanga dakika ya 64.
  Simba SC inaondoka mjini hapa kesho asubuhi kwenda Arusha tayari kwa mchezo wa Jumatano na Oljoro, ambayo leo imeanza Ligi Kuu kwa kufungwa 2-0 nyumbani na Coastal Union.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: RAGE APAA USIKU HUU KWENDA BUJUMBURA KUFUATA ITC ZA WACHEZAJI WARUNDI WA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top