• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 21, 2013

  KWA KIKOSI HIKI CHA KIM POULSEN, SAFARI BADO NDEFU TAIFA STARS

  IMEWEKWA AGOSTI 21, 2013 SAA 12:35 ASUBUHI
  INAFAHAMIKA, timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kwa mara nyingine imetolewa katika kinyang’anyiro cha mashindano yote iliyowania miaka hii miwili, Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zilizofanyika Afrika Kusini mwaka huu, michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee inayofanyika mwakani Afrika Kusini na Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil pia mwakani.  
  Stars imebakiza mechi tu ya kukamilisha ratiba katika Kundi lake kwenye kinyang’anyiro cha tiketi ya Brazil mwakani, dhidi ya Gambia mwezi ujao ugenini.

  Lakini jana, Kocha Mdenmark wa Stars, Kim Poulsen ameita wachezaji 24 kujiandaa kwa mechi dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7, mwaka huu nchini humo, ambao wataripoti kambini Agosti 29, mwaka huu kabla ya saa 1 kamili usiku kwenye hoteli ya Accommondia jijini Dar es Salaam.
  Poulsen karibu ameita kikosi kile kile kilichowania bila mafanikio tiketi za Brazil na Afrika Kusini.
  Walioitwa ni makipa Juma Kaseja (Huru), Mwadini Ali (Azam), Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga) na Aishi Manula (Azam) wakati mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Kevin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba/AS Cannes Ufaransa), Nadir Haroub (Yanga), Erasto Nyoni (Azam), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar) na David Luhende (Yanga).
  Viungo ni Khamis Mcha (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Dilunga (Ruvu Shooting), Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Amri Kiemba (Simba), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga), John Bocco (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Mbwana Samatta (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) na Juma Luizio (Mtibwa Sugar).
  Suala si kuita wachezaji ambao walishindwa kuipatia Stars tiketi za Brazil na Afrika Kusini- bali ni aina ya wachezaji waliopewa jukumu hilo na wakati husika, ukilinganisha na mahitaji halisi ya timu hiyo kwa sasa.
  Baada ya timu kutolewa katika mashindano yote, mijadala mingi ilichukua nafasi na kikubwa kilichoonekana nchi haina wachezaji wa kutosha wenye viwango vya kuchezea timu hiyo.
  Kim alilazimika kuwabembeleza wachezaji ambao hawakutaka kuchezea timu hiyo katika mchezo wa mwisho wa kuwania tiketi ya CHAN na Uganda kwa sababu hakuwa na wachezaji wa kuchukua nafasi zao.
  Viungo Salum Abubakar, Athumani Iddi ‘Chuji’ na mshambuliaji John Bocco ni baadhi ya wachezaji ambao hawakutaka kucheza na Uganda mjini Kampala na waligoma hata kwenda kambini, hadi walipombelezwa wakaenda kwa shingo upande.
  Tayari Poulsen alilalamikia kuwaita mabeki Wazanzibari, Nassor Masoud ‘Chollo’ wa Simba SC na Waziri Salum wa Azam, lakini wote wakagoma kwa kutoa visingizio.
  Hii maana yake, kuna tatizo la wachezaji na tunahitaji kupanua wigo wa wachezaji wa timu ya taifa kuelekea kampeni zijazo. Hapana shaka, baada ya timu kukosa tiketi za Afrika Kusini na Brazil, huu ulikuwa wakati mwafaka kusaka wachezaji wapya wa timu ya taifa kwa kuwapa nafasi wengine wanaofanya vizuri nchini wapate uzoefu.      
  Tunakumbuka katikati ya mwaka kocha Poulsen aliunda kikosi cha pili cha Stars, akisema lengo ni kuandaa wachezaji wa kupandisha katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo ya taifa. 
  Walioitwa ni Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Ali Mustapha ‘Barthez’ (Yanga) ambao ni makipa. Mabeki ni Kessy Hassan (Mtibwa Sugar), Kennan Ngoma (Barnsley FC, Uingereza), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), David Mwantika (Azam), Miraji Adam (Simba), Mohamed Hussein (Kagera Sugar), Waziri Salum (Azam), Samih Nuhu (Azam) na Emily Mgeta (Simba).
  Viungo ni Haruna Chanongo (Simba), Edward Christopher (Simba), Mudathiri Yahya (Azam), William Lucian (Simba), Jonas Mkude (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jimmy Shoji (JKT Ruvu), Abdallah Seseme (Simba), Ramadhan Singano (Simba), Farid Mussa (Azam) na Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar).
  Washambuliaji ni Hussein Javu (Yanga SC), Jerome Lambele (Ashanti United), Zahoro Pazi (Simba SC), Twaha Hussein (Simba SC), Seif Abdallah Karihe (Azam) na Juma Luizio (Mtibwa Sugar).
  Ndiyo, baadhi ya wachezaji wa timu hii unaweza kuona tayari wamepandishwa kikosi cha kwanza- lakini wengi ni ambao wataishia kufanya mazoezi tu pale Karume na hawatasafiri Gambia.
  Kwa kiasi kikubwa wachezaji wa kucheza Gambia watakuwa wale wale ambao wamezoeleka kulingana na kikosi cha Kim cha jana. Tunaujua uwezo wa Samatta na Ulimwengu na hatuna shaka nao kwa sababu pia wanaendelea kukomazwa na Mazembe katika Kombe la Shirikisho Afrika.
  Tunaamini huu ulikuwa wakati mzuri sasa kwa Kim kukigeukia kikosi chake cha pili cha Stars ili kuona uwezo wa kiushindani wa wachezaji wengine katika kuimarisha kikosi chake kitakachoingia kwenye kampeni za AFCON ijayo. 
  Lakini badala yake ameendelea kucheza katika eneo lile lile, maana yake tatizo ambalo lipo kwa sasa litaendelea na Watanzania wataendelea na kilio kile kile siku zote.
  Wakati mwingine ni mambo ya kustaajabisha- inafahamika tunacheza na Gambia kukamilisha Ratiba na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara nayo imesimama kwa zaidi ya wiki kupisha maandalizi ya mchezo huo. Wazi kipindi hiki kingetosha kabisa kuiandaa timu B ya Stars kwa mchezo dhidi ya Gambia.
  Na timu hiyo ya pili ndiyo ambayo ingekuwa inacheza mechi za kirafiki zilizo katika kalenda ya FIFA ili kuwapa uzoefu zaidi wachezaji, na hadi utakapowadia muda wa kampeni za tiketi ya AFCON ijayo, tutakuwa na hazina ya kutosha kidogo ya wachezaji kwa ajili ya Stars, kwa maana ya wale wa sasa na ambao watapatikana baada ya mechi kadhaa kutokana na timu B.
  Lakini kocha Poulsen hajaliona hilo, ameita kuikosi cha nguvu kana kwamba, tukimfunga Gambia tutakwenda popote. Safari bado ndefu kwa kweli kwa mtaji huu. Alamsiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KWA KIKOSI HIKI CHA KIM POULSEN, SAFARI BADO NDEFU TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top