• HABARI MPYA

    Wednesday, August 28, 2013

    UKO WAPI UHALALI WA ADHABU YA MRISHO KHALFAN NGASSA?

    IMEWEKWA AGOSTI 28, 2013 SAA 12:22 ASUBUHI
    MJADALA Mkuu kwa sasa ni adhabu ya mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa kutoka Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Kamati hiyo baada ya kupitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwezi huu, ilimuidhinisha Ngassa kuchezea Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.
    Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa ilibaini kuwa Ngassa alisaini mkataba mwingine Simba, katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam na ikamtaka kurejesha fedha alizopokea Msimbazi, Sh. Milioni 30 na fidia ya asilimia 50, sawa na Sh. Milioni 15, yaani jumla alipe Milioni 45 kwa Simba.
    Kamati pia ikamfungia mechi sita za mashindano na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.

    Tayari Yanga SC imemkosa Ngassa katika mechi mbili, moja ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC waliyoshinda 1-0 na nyingine ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara waliyoshinda 5-1 dhidi ya Ashanti United, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Inafahamika Ngassa alikuwa mchezaji wa Yanga SC tangu mwaka 2007 akitokea Kagera Sugar na mwaka 2010 klabu hiyo ikamuuza Azam FC. Akiwa Azam, Ngassa alionekana kukumbuka maisha ya Jangwani kiasi cha kufikia kuibusu jezi ya timu hiyo akiwa anachezea timu mpya- jambo ambalo likawakera waajiri wake wapya na kuamua kumuuza.
    Azam ilitangaza kumuuza Ngassa, awali kwa Sh. Milioni 50,000 wakiamini kwa kuwa Yanga wanamtaka, watatoa fedha hizo, lakini baadaye dau lake lilipungua hadi Sh. Milioni 25, 000 ambayo waliyotoa Simba SC kuilipa Azam.
    Lakini ajabu bado ikaelezwa Ngassa amechukuliwa kwa mkopo na Simba SC kutoka Azam, hakika ulikuwa mkopo wa aiana yake. Ila mambo yalianza kugeuka baada ya kutokea ofa ya klabu ya El Merreikh ya Sudan ikitaka kumnunua Ngassa Desemba mwaka jana.
    Simba SC walijaribu kutaka kumuuza wao, wakidai ni mchezaji wao halali kwa kuwa walinunua haki za Mkataba wake kutoka Azam- lakini Azam nao wakaibuka na kukana, wakisema walimpeleka Ngassa kwa mkopo Simba SC.
    Inakumbukwa, baada ya Azam kutangaza kumpeleka mchezaji huyo kwa mkopo Simba SC, mwenyewe aliibuka kwenye vyombo vya habari na kukataa, akisema hawezi kukubali kuuzwa kama gunia.
    Wiki moja baadaye, Ngassa akatangazwa kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari kujiunga na Simba SC na yeye mwenyewe akasema, soka ni ajira yake, anaangalia maslahi. Simba SC wamemtekelezea mahitaji yake, amekubali kujiunga nao. 
    Lakini Mkataba wa Ngassa na Simba SC haukuwahi kuonyeshwa zaidi ya mchezaji huyo kuonekana akisani Simba SC akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe na ikaelezwa mbali na fedha walizolipwa Azam, naye alipewa Milioni 18 na gari yenye thamani ya Sh. Milioni 12, jumla Milioni 30.
    Wakati msimu uliopita ukielekea ukingoni, ndipo tetesi za  Ngassa kurejea Yanga SC zikaanza na ndipo Simba SC wakaanza kusema, mchezaji huyo hawezi kurejea Jangwani, kwa kuwa pamoja na Mkataba wa mkopo kutoka Azam, walimsainisha Mkataba mpya wa mwaka mmoja.
    Ni hawa Simba SC ambao awali wakati wa sakata la Merreikh walisema walinunua haki zake zote kutoka Azam na wakasema ili, kujihakikishia awe wao wa kudumu, wakampa Mkataba mpya wa mwaka zaidi.
    Na hapa ndipo yalipolalia malalamiko ya Yanga SC, kwamba Simba SC ilimsainisha Mkataba mchezaji huyo akiwa ndani ya Mkataba mwingine na Azam FC na akiwa amepelekwa kwa mkopo Simba SC, jambo ambalo ni kinyume na kanuni na sharia za usajili nchini.
    Lakini kwa mtazamo wa Simba SC, wao wanaamini walimsainisha Ngassa ili kumuongezea Mkataba baada ya kununua haki zake kutoka Azam. Kweli kuna utata, kama waliuziwa haki za mchezaji na Azam, iweje walishindwa kumuuza wao wenyewe Sudan?
    Ajabu, Ngassa aliposaini Yanga SC, TFF wakasahau kwamba wao wenyewe walisema mchezaji huyo ni wa Azam na alikuwa anacheza Simba SC kwa mkopo, wakasema wanautambua Mkataba wake na Wekundu wa Msimbazi. 
    Na bila shaka huo ndio ulikuwa mwongozo kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF hata ikaamua kuchukua hatua ilizochukua. Kweli hapa kuna utata, na hata kama kweli mchezaji ana makosa, lakini kwa namna ambavyo kesi yake iliendeshwa, kuna mapungufu.
    Kinachojitokeza hapa ni kesi ya uaminifu kati ya Simba SC na Ngassa, kuna mmoja hapa anadanganya, sasa ni nani? Simba au Ngassa? Na kwa swali hili ndipo unapoona umuhimu wa Ngassa na Simba SC kuitwa katika kikao cha Kamati ya Maadili kutoa ushahidi wao, je Kamati hiyo ilifanya hivyo? 
    Na kama haikufanya hivyo ni kwa sababu gani? Na uhalali wa adhabu ya Ngassa unatoka wapi kwa mtaji huu? Yanga SC wana hoja. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: UKO WAPI UHALALI WA ADHABU YA MRISHO KHALFAN NGASSA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top