• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 26, 2013

  WAKALI WA SIMBA SC KUTOKA BURUNDI KUTAMBULISHWA JUMAPILI DAR ES SALAAM KWA MCHEZO SAFI WA KIRAFIKI

  Na Prince Akbar, IMEWEKWA AGOSTI 26, 2013 SAA 8:40 MCHANA
  BAADA ya kupatiwa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC), wachezaji wapya wa Simba SC, Warundi, beki Kaze Gilbert na mshambuliaji Tambwe Amisi watatambulishwa mbele ya mashabiki wa timu hiyo mjini Dar es Salaam Jumapili wiki hii kwa mchezo maalum wa kirafiki dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar, Uwanja wa Taifa.  
  Mwandaaji wa mchezo huo, George Wakuganda amesema mchezo huo ni maalum kwa wapenzi wa Simba SC wa Dar es Salaam kuwashuhudia nyota hao wakiichezea timu yao kwa mara ya kwanza baada ya kupata ITC. 
  Mwenyekiti huyo wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage alilazimika kwenda Burundi kufuata ITC za wachezaji hao mwishoni mwa wiki baada ya kuona zinachelwa kufika nchini, hivyo kuwachelewesha pia kuanza kazi.
  Watatambulishwa Jumapili; Kaze Gilbert kulia akiwa na Tambwe Amisi
   

  Rage aliondoka Dar es Salaam Jumamosi usiku na ilimchukua chini ya saa 24 kuweza kufanikisha suala hilo. Katika taarifa yake kwa wana Simba, Mbunge huyo wa Tabora Mjini alisema amelazimika kuingilia kati suala hilo kwa sababu lilihusu baadhi ya taratibu muhimu za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na ukweli kwamba viongozi wa Vital’O, klabu waliyotoka wachezaji hao hawakuwa mjni na hivyo kuchelewa kwao kungeigharimu Simba.
  “Kila walipokuwa wakipigiwa simu kwa takribani siku tatu mfululizo walikuwa wakisema kwamba wako milimani. Sasa hawa watu wa Burundi wakikwambia wako milimani wanamaanisha wameenda kijijini kwao. Kuongea kwa simu pekee kusingetosha na ndiyo Kamati ya Utendaji ya Simba iliomba niende mwenyewe Burundi ili suala hili liishe,” alisema.
  Hiyo inakuwa mara ya pili kwa Rage, ambaye ana uzoefu wa kuongoza soka kwa zaidi ya miongo mitatu, kuingilia kati suala la uhamisho wa wachezaji wa kimataifa. Miaka miwili iliyopita, Mwenyekiti huyo alilazimika pia kusafiri kwenda nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kushughulikia uhamisho wa mchezaji Gervais Kago ambao nao ulikuwa na matatizo.
  Kutokana na kupatikana kwa ITC hizo, Kaze na Tambwe sasa wataruhusiwa kucheza katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya JKT OIljoro ya Arusha iliyopangwa kufanyika Jumatano ijayo mjini Arusha. Klabu ya Simba tayari imewakatia wachezaji hao vibali vya kufanya kazi hapa nchini.
  Wachezaji wengine wa kigeni wa Simba, Joeph Owino na Abel Dhaira, walicheza katika mechi ya jana kutokana na kukamilisha taratibu zote za uhamisho na kuwa na vibali vya kufanya kazi hapa nchini
  Sasa wachezaji hao wataichezea Simba SC katika mechi ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha Jumatano, baada ya juzi kukwama kucheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya wenyeji, Rhino Rangers mjini Tabora.  
  Wachezaji hao waliosajiliwa kutoka mabingwa wapya wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Vital’O ya kwao, juzi walikuwapo Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi kuishuhudia timu yao ikilazimishwa sare ya 2-2 na Rhino.
  Kocha Mkuu wa Simba SC, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ alisema kukosekana kwa wachezaji hao jana kulichangia matokeo ya sare kwa timu yake.
  Kibadeni, ambaye pia alisema kipa Mganda Abbel Dhaira aliwaangusha juzi kwa kufungwa mabao rahisi, alisema aliwaandaa wachezaji hao kwa ajili ya kucheza siku hiyo, hivyo kuwakosa ilimvurugia mipango yake.
  Simba SC ililazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya juzi. 
  Mabao yote ya Simba SC yalifungwa na kiungo Jonas Mkude dakika za 10 na 38 kwa penalti, wakati ya Rhino yalifungwa na Iman Noel dakika 36 na Saad Kipanga dakika ya 64.
  Simba SC iliondoka jana Tabora kwenda Arusha tayari kwa mchezo wa Jumatano na Oljoro, ambayo juzi ilianza Ligi Kuu kwa kufungwa 2-0 nyumbani na Coastal Union.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: WAKALI WA SIMBA SC KUTOKA BURUNDI KUTAMBULISHWA JUMAPILI DAR ES SALAAM KWA MCHEZO SAFI WA KIRAFIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top