• HABARI MPYA

  Jumapili, Agosti 25, 2013

  RAGE STERLING AINGIA BUJUMBURA NA KUKAMATA ITC ZA WAKALI TAMBWE NA KAZE

  Na Mahmoud Zubeiry, Tabora IMEWEKWA AGOSTI 24, 2013 SAA 9:20 ALASIRI
  RAGE sterling. Unaweza kusema hivyo baada ya Mwenyekiti huyo wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage kufanikiwa kupata Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) za wachezaji wake Warundi, Kaze Gilbert na Tambwe Amisi.  
  Rage aliondoka Dar es Salaam jana usiku na imechukua chini ya saa 24 kuweka kufanikisha suala hilo. Katika taarifa yake kwa wana Simba, Mbunge huyo wa Tabora Mjini alisema amelazimika kuingilia kati suala hilo kwa sababu lilihusu baadhi ya taratibu muhimu za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na ukweli kwamba viongozi wa Vitalo, klabu waliyotoka wachezaji hao hawakuwa mjni na hivyo kuchelewa kwao kungeigharimu Simba.
  “Kila walipokuwa wakipigiwa simu kwa takribani siku tatu mfululizo walikuwa wakisema kwamba wako milimani. Sasa hawa watu wa Burundi wakikwambia wako milimani wanamaanisha wameenda kijijini kwao. Kuongea kwa simu pekee kusingetosha na ndiyo Kamati ya Utendaji ya Simba iliomba niende mwenyewe Burundi ili suala hili liishe,” alisema.
  Sterling; Rage amepata ITC za Tambwe na Kaze na sasa watacheza Jumatano

  Hii ni mara ya pili kwa Rage, ambaye ana uzoefu wa kuongoza soka kwa zaidi ya miongo mitatu, kuingilia kati suala la uhamisho wa wachezaji wa kimataifa. Miaka miwili iliyopita, Mwenyekiti huyo alilazimika pia kusafiri kwenda nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kushughulikia uhamisho wa mchezaji Gervais Kago ambao nao ulikuwa na matatizo.
  Kutokana na kupatikana kwa ITC hizo, Kaze na Tambwe sasa wataruhusiwa kucheza katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya JKT OIljoro ya Arusha iliyopangwa kufanyika Jumatano ijayo mjini Arusha. Klabu ya Simba tayari imewakatia wachezaji hao vibali vya kufanya kazi hapa nchini.
  Wachezaji wengine wa kigeni wa Simba, Joeph Owino na Abel Dhaira, walicheza katika mechi ya jana kutokana na kukamilisha taratibu zote za uhamisho na kuwa na vibali vya kufanya kazi hapa nchini
  Sasa wachezaji hao wataichezea Simba SC katika mechi ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha Jumatano, baada ya jana kukwama kucheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya wenyeji, Rhino Rangers mjini Tabora.  
  Wachezaji hao waliosajiliwa kutoka mabingwa wapya wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Vital’O ya kwao, jana walikuwapo Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi kuishuhudia timu yao ikilazimishwa sare ya 2-2 na Rhino.
  Kocha Mkuu wa Simba SC, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ alisema kukosekana kwa wachezaji hao jana kulichangia matokeo ya sare kwa timu yake.
  Kibadeni, ambaye pia alisema kipa Mganda Abbel Dhaira aliwaangusha jana kwa kufungwa mabao rahisi, alisema aliwaandaa wachezaji hao kwa ajili ya kucheza jana, hivyo kuwakosa ilimvurugia mipango yake.
  “Nilitegemea sana kuwatumia wale mabwana leo (jana), lakini kwa bahati mbaya, ITC zao zimechelewa kufika na tumeshindwa kuwatumia, kwa kweli imeniangusha sana,”alisema.
  Simba SC ililazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya jana. 
  Mabao yote ya Simba SC yalifungwa na kiungo Jonas Mkude dakika za 10 na 38 kwa penalti, wakati ya Rhino yalifungwa na Iman Noel dakika 36 na Saad Kipanga dakika ya 64.
  Simba SC imeondoka leo mjini hapa kwenda Arusha tayari kwa mchezo wa Jumatano na Oljoro, ambayo jana ilianza Ligi Kuu kwa kufungwa 2-0 nyumbani na Coastal Union.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: RAGE STERLING AINGIA BUJUMBURA NA KUKAMATA ITC ZA WAKALI TAMBWE NA KAZE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top