• HABARI MPYA

  Jumapili, Agosti 25, 2013

  SIMBA SC WAANZA KUMKUMBUKA KASEJA BAADA YA DHAIRA KUBORONGA JANA

  Na Mahmoud Zubeiry, Tabora IMEWEKWA AGOSTI 25, 2013 SAA 5:27 ASUBUHI
  MASHABIKI wa Simba SC jana walimkumbuka kipa wao wa kwanza wa muda mrefu, Juma Kaseja kufuatia kipa wao wa kwanza wa sasa, Abbel Dhaira kufungwa mabao rahisi katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Rhino Rangers, Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini hapa, timu hizo zikitoka 2-2.  
  Baada ya mchezo huo, mashabiki ambao wametoka Dar es Salaam kuja kuisapoti timu mjini hapa walianza kulalamikia uamuzi wa uongozi kumtema Kaseja, kama ulikuja mapema mno.
  Abbel Dhaira jana kafungwa mabao rahisi

  Na wakazama ndani zaidi kwa kusema, baadhi ya viongozi walipandikiza chuki zisizo na tija kati ya Kaseja na mashabiki, hadi kipa huyo akawa anachukiwa kupita kiasi, hatimaye kuonekana maamuzi ya kutemwa ni sahihi.
  Hata kocha Mkuu wa Simba SC, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ alisikitishwa na kipa huyo Mganda akisema Abbel Dhaira amewaangusha kwa kufungwa mabao rahisi.
  Dhaira alifungwa mabao yote ya mipira ya adhabu kutoka umbali wa zaidi ya mita 20 katika mchezo wa jana, ingawa naye alionekana kuwalalamikia mabeki wake kwamba walimpoteza maboya walipopanga ukuta wao ovyo.
  Anamkumbuka Kaseja; Kocha Abdallah KIbadeni jana Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora

  Wakati wa mapumziko, Dhaira alikuwa akizozana na Mganda mwenzake, beki Joseph Owino wakati wakirejea vyumbani kutokana na bao la kwanza na baada ya mechi kipa huyo hakutaka kuzungumza na yeyote alielekea moja kwa moja kwenye basi akiwa amekasirika.
  Mabao yote ya Simba SC jana yalifungwa na kiungo Jonas Mkude dakika za 10 na 38 kwa penalti, wakati ya Rhino yalifungwa na Iman Noel dakika 36 na Saad Kipanga dakika ya 64.
  Kaseja alitemwa Simba SC mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuitumikia klabu hiyo tangu mwaka 2003 alipojiunga nayo akitokea Moro United ya Morogoro, hoja ikiwa kiwango chake kimeshuka.
  Atarudishwa? Simba SC wameanza kumkumbuka Juma Kaseja 

  Katika kipindi chote hicho, Kaseja aliondoka mwaka mmoja tu kwenda kuidakia Yanga msimu wa 2009 na baada ya kumaliza Mkataba wake mwaka mmoja, alirejea Msimbazi.
  Pamoja na kutemwa Simba SC na sasa akiwa hana timu, Kaseja ameendelea kuitwa katika kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na pia akiendelea kuwa kipa chaguo la kwanza mbele ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen.
  Wanamkumbuka Kaseja; Mashabiki wa Simba waliotoka Dar es Salaam, wakiwa Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi jana
  Wakati Dhaira jana akifungwa mabao rahisi, hata kipa wa pili, Andrew Ntalla bado hajaonyesha kuwa tayari sana kwa majukumu mazito katika klabu hiyo- maana yake anahitaji muda.
  Na kama Dhaira ataendelea kufungwa mabao rahisi, kuna uwezekano Simba SC ikamuangukia Kaseja na kumrejesha katika dirisha dogo la usajili Januari, iwapo naye ataendelea kufanya vizuri Taifa Stars.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA SC WAANZA KUMKUMBUKA KASEJA BAADA YA DHAIRA KUBORONGA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top