• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 22, 2013

  AS CANNES YAMWAGIA SIFA KEDEKEDE KAPOMBE, YASEMA ATAWABEBA UFARANSA..YAMPA UZI KAMA WA MSIMBAZI

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA AGOSTI 22, 2013 SAA 1:05 USIKU
  RASMI, klabu ya Daraja la Nne Ufaransa, AS Cannes imetangaza katika tovuti yake kwamba katika kujiimarisha ili kutoka katika kipindi kigumu, imeboresha kikosi chake kwa kumsajili kiungo Mtanzania, Shomari Salum Kapombe.
  Klabu hiyo imesema hiyo pia itakuwa fursa kwa mchezaji huyo kutoka Simba SC ya Tanzania kujipatia uzoefu wa kimataifa akiwa na Weupe hao Ufaransa.
  Imemuelezea Kapombe, kama kinda mwenye umri wa miaka 21, ambaye hadi sasa amekwishachezea mechi 14 timu yake ya taifa, Taifa Stars pamoja na kumkabidhi jezi kuanza rasmi mazoezi na wenzake. Na imevutiwa naye zaidi baada ya wasifu wake kusema anaweza kucheza nafasi nyingine pia, zikiwemo za ulinzi, hivyo atakuwa msaada mkubwa kwa kocha Jean-Marc Pilorget msimu huu. 
  Uzi kama wa Msimbazi; Shomary Kapombe katika jezi ya timu yake mpya Ufaransa
  Imesema viongozi wanafanya jitihada kubwa kuhakikisha wanainua kiwango chake haraka ili aweze kufanikiwa zaidi Ulaya.
  Wiki iliyopita, Simba SC ilitangaza kumuunganisha Kapombe na AS Cannes kwa mkataba wa maridhiano maalum.
  Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage, alisema kwamba katika mkataba huo mpya na wa aina yake kuwahi kufanywa na klabu yoyote ya Tanzania, Simba imekubali mchezaji huyo achezee timu hiyo iliyo katika ligi daraja la nne la Ufaransa kwa makubaliano ya kumtafutia timu ya kucheza ndani ya miaka miwili kutoka sasa.
  Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), amesema timu hiyo itamgharimia Kapombe kwa kila kitu wakati atakapokuwa nchini Ufaransa na endapo atauzwa kwenda katika timu nyingine yoyote, Simba itapata gawio lake kupitia mauzo hayo na lengo la mchezaji huyo kubaki Ufaransa ni pia kumtengeneza awe bora zaidi kuliko alivyo sasa.
  “Kwenye makubaliano hayo, Simba haitapata chochote kwa sasa. Isipokuwa endapo Kapombe atapata timu, Simba itapata mgawo wake kutoka katika mauzo hayo. Makocha wa Ulaya wamebaini kwamba Shomari ni mchezaji mzuri sana lakini anahitaji kuboreshewa vitu vichache kabla hajawa mchezaji mkubwa wa kutumainiwa na vilabu vikubwa,” alisema Rage.
  Rage alisema katika mkataba huo mpya wa Kapombe, Simba imeangalia zaidi maslahi ya taifa na ya mchezaji kuliko ya klabu kwa vile kama mchezaji huyo atapata nafasi Ulaya, hilo litafungua milango kwa wachezaji wengi wa Kitanzania ambao kwa sasa hawapati fursa Ulaya.
  Wakala wa Kapombe, Denis Kadito, alisema ingawa Kapombe ameonekana kuwa mchezaji mzuri, kutofahamika kwa jina la Tanzania kumekuwa kikwazo kikubwa kwa kupata kwake nafasi ya moja kwa moja na ndiyo maana 

  WASIFU WA SHOMARI SALUM KAPOMBE...

  “Alianza soka mwaka 1999 akiwa ana umri wa miaka saba katika timu ya watoto waokota mipira wa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro- maarufu kama Jamhuri Ball Boys...
  Alipofikisha umri wa miaka 14 akajiunga na akademi maarufu mkoani Morogoro, Moro Kids wakati huo akicheza nafasi ya ushambuliaji. Lakini kocha wake wakati huo, `Mau’ akambadili hadi kuwa kiungo.
  Akafanikiwa zaidi na kwenda kuiwakilisha Morogoro katika mashindano ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Copa Coca Cola akiwa Nahodha mwaka 2008...
  Kutoka hapo akasajiliwa katika kikosi cha vijana cha Simba SC na msimu wake wa kwanza tu 2011 akapandishwa timu ya wakubwa. Aliitwa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, baadaye timu ya wakubwa mwaka jana na sasa ni tegemeo la timu hiyo chini ya kocha Mdenmark, Kim Pouslen.
  “Ofa hii ya Cannes ni nzuri kwa sababu timu hiyo huwa inacheza na timu za akiba za vilabu vyote vinavyoshiriki katika Ligi Kuu ya Ufaransa na hivyo atakuwa anaonwa na mawakala wa timu kubwa kila wiki. Hii itamsaidia kupata timu kubwa mapema ndani ya msimu mmoja kutoka sasa,”AS Cannes ni mojawapo ya vilabu vikubwa nchini Ufaransa na ni maarufu kwa kuibua vipaji vikubwa. Miongoni mwa nyota maarufu wa Ufaransa waliowahi kupita katika klabu hiyo ni Patrick Vieira, Zinedine Zidane na Luis Hernandez.
  Klabu hiyo inafahamika kwa kuwa na miundombinu imara ya kumwezesha mwanasoka kijana kukuza uwezo wake na ni matarajio ya Simba Sports Club, Kadito, Cannes na Kapombe mwenyewe kwamba atakuwa mchezaji bora zaidi kuliko sasa katika kipindi cha mwaka mmoja kutoka sasa.
  Kutokana na mkataba huo wa Kapombe na Cannes, Simba sasa imeongeza mkataba wake na mchezaji huyo kwa muda wa miaka mitatu zaidi, kwa vile mkataba wake wa sasa unamalizika Aprili mwakani. 
  Kama Kapombe hatafanikiwa kupata timu katika kipindi cha miaka miwili kutoka sasa, atarejea katika klabu ya Simba kuendelea na majukumu yake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: AS CANNES YAMWAGIA SIFA KEDEKEDE KAPOMBE, YASEMA ATAWABEBA UFARANSA..YAMPA UZI KAMA WA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top