• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 19, 2013

  SIMBA SC YASEMA MOMBEKI ATACHEZA LIGI KUU...NA MKALI WA MABAO AFRIKA MASHARIKI ANATUA LEO, KIKOSI CHA UBINGWA KIMEKAMILIKA

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA AGOSTI 19, 2013 SAA 5: 24 ASUBUHI
  WAKATI mshambuliaji mpya wa Simba SC, Tambwe Amisi anatarajiwa kuwasili nchini mchana wa leo, klabu hiyo imewaondoa hofu mashabiki wake kuhusu mpachika mabao wao hodari kwa sasa, Betram Mombeki.
  Simba SC imesema kwamba Mombeki atacheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa sababu hajawekewa pingamizi na klabu yoyote.
  Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba hawajaona pingamizi lolote juu ya Mombeki, hivyo atacheza Ligi Kuu.
  “Sisi hatujaona pingamizi lolote kimaandishi, kama ilikuwa inazungumzwa, basi yalikuwa maneno tu na Mombeki atacheza Ligi Kuu,”alisema Kinesi.
  Atacheza Ligi Kuu; Betram Mombeki hajawekewa pingamizi la maandishi, ni la mdomo tu


  Mombeki alisajiliwa na Simba SC majira haya ya joto akisema alikuwa Marekani na aliwahi kuchezea Pamba FC ya Mwanza hapo kabla. Lakini klabu ya Pamba, ikakariwa na vyombo vya Habari ikilalamika Simba SC kutofuata taratibu za kumsajili mchezaji wao. 
  Pamba ilidai Mombeki alisaini kwao na kuwachezea katika Ligi ya Mkoa wa Mwanza akitokea Marekani, lakini baadaye Simba wakamteka bila kufuata taratibu za kumhamisha.
  Kuhusu mshambuliaji mwingine mpya, Tambwe Amisi ambaye ni mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Kinesi alisema anatua mchana wa leo kutoka kwao Burundi.
  Mshambuliaji huyo wa Vital’O ya Burundi pamoja na kusajiliwa miezi miwili iliyopita, lakini hajawahi hata kufanya mazoezi na Wekundu hao wa Msimbazi.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA SC YASEMA MOMBEKI ATACHEZA LIGI KUU...NA MKALI WA MABAO AFRIKA MASHARIKI ANATUA LEO, KIKOSI CHA UBINGWA KIMEKAMILIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top