• HABARI MPYA

  Jumamosi, Agosti 24, 2013

  MADUDU HAYA UCHAGUZI TFF, YETU MACHO!

  IMEWEKWA AGOSTI 24, 2013 SAA 3:22 ASUBUHI
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) linaendelea na mchakato wa uchaguzi wake Mkuu, katika nafasi mbalimbali za uongozi, na zoezi la uchukuaji fomu lilikamilika Agosti 20, 2013.
  Fomu zilichukuliwa kwa fedha kutegemeana na nafasi unayogombea- kwa nafasi ya Mwenyekiti Sh 500,000, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi Sh 300,000 na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni sh 200,000.
  Kwa mtazamo wangu, sioni sababu kwa nini hizi fomu ziwe ghali kiwango hicho, ilihali hii ni kazi ya kujitolea, isiyo kua na malipo, sijajua lengo la kuzitoa hizi fomu kwa gharama kubwa kiwango hicho.

  Au pengine ni sehemu ya chanzo cha mapato kimojawapo cha kuingizia fedha TFF, yaani kutunisha mfuko au ni kuigharamia Kamati husika ili ijiendeshe yenyewe? 
  Labda sababu nyingine ni kupunguza utitiri wa watu kuchukua fomu, hata wale ambao hawakuwa na sifa stahili na kuipa Kamati kazi kubwa, pia labda kuwa kiongozi TFF ni nafasi kubwa sana kwenye jamii, kwa hiyo hata uchukuaji fomu uendane na nafasi hiyo nk.
  Kwa sababu zozote zile, hapo juu nilizozitaja na nyinginezo, bado kipato cha mwananchi wa Tanzania siyo kikubwa, hasa kwa wadau wenyewe wa mpira, wao kuanzia makocha marefa hata viongozi mbalimbali katika sekta za mpira wa miguu, kwa 500,000 maana yake familia zao zisile kwa miezi kadhaa pengine.
  Hii si haki, hasa kwa wenye mpira wao kuwaweka nje ya uongozi, wakati mwingine ndio sababu mpira wa Tanzania hauendelei, kwani Manahodha wao sio wadau wa mpira.
  Kama lengo ni kupunguza watu wengi wasichukue fomu, kwa kuuita ni utitiri, nayo sio sawa, kwani ni kuua demokrasia kwa kisingizio cha fomu, kwani kuwa na wagombea wengi ndio kuwapa wigo mpana wachaguzi, yaani wapiga kura, kuliko kuwa na wagombea wawili au watatu pengine mgombea mmoja.
  Hali hii si ya bahati mbaya, tatizo tu ni baadhi ya viongozi ndani ya TFF kuingilia mchakato mzima wa uchaguzi, kuhofia kupoteza nafasi zao kutokana na utendaji, pengine kujihisi ni mbovu au baadhi yao wanagombea.
  Kwa hiyo, kuamua kupunguza ushindani kwa makusudi kabisa na pengine wabaki wenyewe bila upinzani.
  TFF imekuwa ikiweka vikwazo chungu nzima, kama mgombea lazima awe digirii- hili liliwaacha wadau wengi wenye uwezo wa kuongoza kuwa nje ya uongozi, wakati hizi nafasi za kuchaguliwa sio za kitaaluma zaidi na hazina uhusiano na hizo digirii, labda wangesema digrii iwe ya taaluma ya michezo. Lakini wemesema ni digirii tu hata kama ni ya upishi, sina maana upishi ni jambo baya, la hasha najaribu tu kuhusisha na uongozi wa mpira wa miguu.
  Sasa leo suala la digirii limeonekana ni kikwazo bado, wameibuka na gharama tena za uchukuaji wa fomu 500,000 kwa watumishi wa kawaida wa Serikali, katika sekta binafsi pia hata waliojiajiri wenyewe, hii si sawa matokeo yake wagombea wanabaki wale wale kila miaka.
  Wameshindwa kuleta mabadiliko sehemu walizoongoza na hawana jipya zaidi ya kuendeleza migogoro tu na kugeuza burudani ya mpira kuwa uwanja wa vita vya maneno, fitina, majungu na kutengeneza makundi mbalimbali katika katika vyama vya mikoa, wilaya na wadau wa mpira kwa ujumla wao.
  Kwa mtazamo huu, mpira Tanzania hautapiga hatua na hakutakuwa na mabadiliko kamwe.
  Mabadiliko haya yaliyopo sasa angalau si kama tulikotoka kwenye magomvi, majungu nk, tutarudi tena huko na dalili zimeanza kujitokeza katika hizi hatua za mchakato mzima wa uchaguzi.
  Rais anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga nampongeza kwa kazi nzuri hasa ya kutangeneza mfumo wa uongozi na utulivu ndani ya mpira wa miguu, ingawa wasaidizi wake wamemwangusha sana katika utendaji wao wa kila siku, ingawa sio wote kwa kuwa aliwaamini sana.
  Kuwaamini wasaidizi ni jambo jema, ila imani isipitilize ukashindwa hata kupitia wanachokifanya kabla hakijaenda kwa walaji hasa kwa maswala ya msingi.
  Nasema tena, Sh. 500,000 ni nyingi mno kwa maisha ya Mtanzania wa kawaida na msitengeneze sheria za kuwabeba baadhi ya watu au kikundi kidogo cha watu.
  Msitengeneze mazingira wagombea kubaki walewale wengine na wana magomvi ya muda mfefu yakiaambatana na wivu, fitina, majungu na makundi- ilitakiwa kuwapa frsa na watu wengine wagombee ili wapiga kura wawe na wigo mpana hata ikiwezekana hawa wagomvi wagomvi watupwe nje ya uongozi kabisa- na si kuwakata katika kamati zenu.

  Tukutane JUMAMOSI IJAYO YUFIKIRI TOFAUTI TENA

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MADUDU HAYA UCHAGUZI TFF, YETU MACHO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top