• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 28, 2013

  HANS POPPE: YANGA WANAMTAFUTIA NGASSA BALAA LA KUONGEZEWA ADHABU

  Na Mahmoud Zubeiry, Tabora, IMEWEKWA AGOSTI 28, 2013 SAA 8:30 MCHANA
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amewaonya Yanga SC kwamba harakati wanazozifanya kwa sasa ni mbaya zaidi kwa Mrisho Khalfan Ngassa, kwani anaweza kuongezewa adhabu iwapo kesi yake itasikilizwa upya. 
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY kutoka Bujumbura, Burundi leo, Hans Poppe amesema kwamba Yanga SC wangekubaliana na uamuzi wa awali wa Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwani ni mzuri mno kwao.
  “Kwa kuwa amesaini mikataba miwili, sheria iko wazi, ni kufungiwa mwaka mmoja. Ni sisi Simba SC ndiyo tuliopaswa kuilalamikia hiyo adhabu na pia maamuzi ya kikao hicho hayana rufaa na wakikaa kuipitia upya kesi yake, anaweza kuongezewa adhabu,”.
  Wanamtafutia balaa Ngassa; Hans Poppe amewaonya Yanga SC na harakati zao

  “Na kuhusu kusaini Mkataba kabla ya mwingine kwisha, unaruhusiwa kwa idhini ya wanaommiliki, na Yanga hawakuwa wanammiliki Ngassa wakati tunamsaini, sasa tatizo liko wapi?,”alihoji Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi wa la Wananchi Tanzania (JWTZ).
  Kamati ya Mgongolwa, baada ya kupitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwezi huu, ilimuidhinisha Ngassa kuchezea Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.
  Hata hivyo, Kamati hiyo ilibaini kuwa Ngassa alisaini mkataba mwingine Simba, katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam na ikamtaka kurejesha fedha alizopokea Msimbazi, Sh. Milioni 30 na fidia ya asilimia 50, sawa na Sh. Milioni 15, yaani jumla alipe Milioni 45 kwa Simba.
  Utaongezewa adhabu dogo; Ngassa anaweza kuongezewa adhabu kesi yake ikisilizwa upya kwa mujibu wa Hans Poppe

  Kamati pia ikamfungia mechi sita za mashindano na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.
  Kufuatia adhabu hiyo, Yanga SC ambayo tayari imemkosa Ngassa katika mechi mbili, moja ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC waliyoshinda 1-0 na nyingine ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara waliyoshinda 5-1 dhidi ya Ashanti United, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imekata Rufaa TFF kupinga.
  Katika Rufaa yao, hoja ya msingi ni kwamba Simba SC ilifanya makosa kuingia Mkataba na Ngassa akiwa ndani ya Mkataba wa Azam FC- hivyo ndiyo waliostahili kuadhibiwa na si mchezaji. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: HANS POPPE: YANGA WANAMTAFUTIA NGASSA BALAA LA KUONGEZEWA ADHABU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top