• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 22, 2013

  BABBI ATUA KMKM BAADA YA KUIPIGA CHINI AZAM

  Na Prince Akbar, IMEWEKWA AGOSTI 22, 2013 SAA 11: 48 ALFAJIRI
  KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Kassim Sadallah, maarufu kama Babi au Ballack wa Unguja amejiunga na mabingwa wa zamani wa Ligi ya Muungano, KMKM ya Zanzibar kwa ajili ya Ligi Kuu ya Zanzibar msimu ujao. 
  Babbi anajiunga na timu hiyo ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo baada ya kudai kugoma kuongeza Mkataba wake na Azam FC, kufuatia wa awali kumalizika mwishoni mwa msimu.
  “Namshukuru Mungu, mimi ni mzima wa afya, nimesaini Mkataba na KMKM, mabingwa wa soka Zanzibar na timu inayoshiriki mashindano ya kimataifa na mashindano mbalimbali, ikiongozwa na kocha mzoefu na mwenye ujuzi wa hali ya juu, Ally Bushiri,”alisema Babbi.
  Sasa KMKM; Babbi amerudi nyumbani

  Kiungo huyo mwenye umbo zuri la kimichezo, alisema anatoa shukrani zake za dhati kwa uongozi wa KMKM kwa kumaliza zoezi la usajili kati yake na wao.
  “Na ninapenda kuwashukuru wapenzi wote wa KMKM, kwa kuniunga mkono pamoja na uongozi wa juu. Ninafurahi zaidi kwa vile nipo nyumbani karibu na familia yangu na biashara zangu za hapa na pale, asanteni sana Watanzania wote,”alisema Babbi.
  Miezi miwili iliyopita, Babbi alisema alikataa kuongeza Mkataba, licha ya kuombwa mara tatu na uongozi wa klabu hiyo, ingawa hakusema sababu za kukataa. 
  “Naona wengi wananitumia sms..kwa kujua habari za Azam..labda kwa ufupi tu ..niwaambie, kwa urefu nitawambia siku nyengine..mimi sipo Azam. Mkataba wangu umeisha na sikutaka kuongeza, mfahamu hivyo, la kama ningetaka, nigesaini, ila sikutaka, maana nimefanya mazugumzo na Azam mara tatu, hatukuafikiana, mimi hawajaniacha, ila nimewaacha wao,”alisema Babi.
  Babbi alijiunga na Azam msimu uliopita akitokea Vietnam alipokuwa anacheza soka ya kulipwa. Kabla ya hapo, alichezea Yanga SC ya Dar es Salaam na Mtibwa Sugar ya Morogoro akitokea kwao Zanzibar.   
  Babi alikuwa tegemeo la timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kati ya mwaka 2005 na 2011 na zaidi alikuwa anaibeba timu hiyo enzi za kocha Mbrazil, Marcio Maximo.
  Aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam, Septemba 1, mwaka 2007 wakati Stars ikiilaza 1-0 Uganda katika mchezo maalum wa kirafiki wa ufunguzi wa Uwanja huo.
  Sifa yake kubwa ni mashuti makali na ndiyo yaliyomfanya apewe jina Ballack, akifananishwa na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani na Chelsea, Michael Ballack. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: BABBI ATUA KMKM BAADA YA KUIPIGA CHINI AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top