• HABARI MPYA

    Monday, August 19, 2013

    ZFA IANZSHE KANUNI ZA KUPIMA AFYA ZA WACHEZAJI WANAOSAJILIWA

    IMEWEKWA AGOSTI 19, 2013 SAA 4:15 ASUBUHI
    CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa, tayari kimetangaza tarehe ya kuanza kwa ligi kuu ya soka inayodhaminiwa na kampuni ya TBL kupitia kinywaji chake cha Grand Malt kwa msimu wa mwaka 2013/2014.
    Ligi hiyo imepangwa kuanza Septemba 5, mwaka huu katika viwanja vya Amaan Unguja na Gombani Pemba.
    Huo utakuwa msimu wa pili tangu ligi hiyo ilipopata mdhamini huyo, ambaye amekubali kuibeba kwa misimu mitatu kuanzia ule uliopita wa 2012/2013.
    Kwa kuwa ZFA ya sasa chini ya Rais wake mpya Ravia Idarous Faina imedhamiria kunyamazisha kilio cha wadau juu ya kuporomoka kwa kiwango cha soka, ninapenda niipe ushauri wa bure juu ya umuhimu wa kujenga timu zilizo imara.

    Ingawa tayari muda wa zoezi la usajili umemalizika na timu zote zimeshawasilisha wachezaji zinaotarajia kuwatumia katika msimu ujao wa ligi kuu, ushauri wangu huu unaweza kufanyiwa kazi mwaka mwengine, au hata wakati wa dirisha dogo.
    Kujua afya za mchezaji kabla timu haijaamua kuingia mkataba naye, ni jambo muhimu sana na linalohitaji kuchukuliwa kwa uzito unaostahili.
    Hili ni sharti la kwanza katika nchi nyengine zikiwemo za Ulaya au hata bara la Afrika, ambalo sisi Zanzibar bado hatujaona umuhimu wake.
    Sina uhakika, lakini ninadhani utaratibu huu hauko hata Shirikisho la Soka Tanzania Bara (TFF), kwani klabu huamua kusajili wachezaji na kuwapima kiwango cha uchezaji uwanjani tu bila kwanza kuwapima afya zao.
    Kubwa ambalo klabu zinajali, ni namna mchezaji huyo anavyoweza kuwafurahisha katika kumiliki mpira, kupiga danadana na mbinu nyengine za uchezaji kuliko kufahamu afya yake.
    Basi si vibaya kama nasi tutaiga mambo mazuri yanayofanywa na nchi nyengine zilizoendelea kisoka, kama hili la kuwapima wachezaji wanaosajiliwa kuzichezea klabu mbalimbali.
    Kwa vile michezo ikiwemo mpira wa miguu ni ajira, ni lazima zitumike taratibu zote za msingi pale klabu inapokusudia kusajili mchezaji na kumpa ajira ya kuitumikia timu husika.
    Sote tunafahamu kwamba muajiri yeyote huhitaji watu wenye afya njema ili wamsaidie katika kufanya kazi iwe za kuzalisha, za kiutawala au za aina yoyote nyengine.
    Ili hili liwezekane, lazima kwanza mfanyakazi huyo afanyiwe vipimo vya afya na baadae daktari athibitishe kwamba ni mzima na hapo ndipo apewe mkataba.
    Sina haja ya kuelezea wenzetu wanafanya nini, kwani sote tunafahamu kwa kufuatilia taarifa za usajili katika klabu mbalimbali za soka barani Ulaya na katika nchi nyengine duniani.
    Kupima afya kuna faida kubwa kwa timu na hata kwa mchezaji, kwani huenda mchezaji huyo ana matatizo makubwa ya kiafya ambayo bado hayajajichomoza, hivyo vipimo ndivyo vitakavyomsaidia kubaini ya ndani na kuanza tiba mapema.
    Ama kwa upande wa klabu inaweza kunufaika kwa kutoingia hasara ya kumlipa mchezaji fedha nyingi kabla haijatambua kama ni mzima wa afya au la.
    Napenda nitolee mfano kadhia ya mchezaji Chukwudi kutoka Nigeria ambaye aliletwa nchini na Yanga wiki kadhaa zilizopita, lakini akabainika ana matatizo ya kiafya na kutokana na majeraha ya zamani yaliyochangia ashindwe kuonesha kiwango kizuri na kumridhisha kocha.
    Yanga ililazimika kumrejesha kwao Mnigeria huyo na kuangalia mbele.
    Ninashangaa hapa Zanzibar wachezaji wanahamishwa kutoka klabu moja kwenda nyengine na kusajliwa bila kufanyiwa vipimo ili klabu ijiridhishe.
    Timu ikishavutiwa na mchezaji kwa kumuona uwanjani akicheza, huwa basi tena kinachofuata ni jitihada za kumshawishi yeye na klabu anayochezea imuachie na akifika hakuna upimaji wa afya kazi moja tu nayo ni kucheza soka.
    Kuanzia sasa lazima ZFA inapotoa fomu za uhamisho na usajili kwa mchezaji, pia iziambatanishe na fomu za kwenda hospitali ili kupimwa afya.
    Kama klabu haitarejesha fomu za vipimo vya afya sambamba na za usajili, ZFA isiruhsu mchezaji husika kuichezea timu hiyo.
    Na katika hili la kuhakikisha wachezaji wanakuwa na afya nzuri, ZFA izilazimishe klabu za ligi kuu na nyengine, ziwe na mikoba ya dawa za huduma ya kwanza ili wachezaji wanaoumia viwanjani waweze kuhudumiwa haraka.
    Na lazima timu ziwe na wataalamu wa afya wenye ujuzi wa kuwatibu wachezaji, na sio wababaishaji ambao wanaweza kusababisha madhara badala ya kutibu.
    Ule mtindo wa mchezaji kuumia akapelekewa kopo la maji ukomeshwe, kwani hiyo si dawa ya kutuliza maumivu aliyopapata.
    Ninalisema hili kwani imezoeleka kuona mchezaji ameumia na wasaidizi wa benchi la ufundi kukimbia mbio uwanjani wakiwa na makopo au madumu ya maji, hali inayoonesha kuwa wanakwenda kuwasaidia wenzake wenye kiu sio kumtibu mchezaji huyo.
    Lazima timu ziache kujiendesha kizamani na zifuate taratibu wa kitaalamu, kwani afya za wachezaji wanaowasajili ni muhimu sana zijulikane na pale penye matatizo yatibiwe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: ZFA IANZSHE KANUNI ZA KUPIMA AFYA ZA WACHEZAJI WANAOSAJILIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top