• HABARI MPYA

    Tuesday, August 27, 2013

    WATOTO TABORA WAMUAMBIA BOCCO; "TUNAKUPENDA WEWE, LAKINI SISI NI RHINO"

    Na Mahmoud Zubeiry, Tabora, IMEWEKWA AGOSTI 27, 2013 SAA 2:45 USIKU
    MASHABIKI wa soka watoto mjini hapa, leo wamemtolea kali mshambuliaji wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ baada ya kumuambia wanampenda yeye, lakini wao ni Rhino.
    Azam ilikuwa inafanya mazoezi jioni ya leo Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Rhino Rangers na mashabiki waliomiminika kwa wingi walikuwa wanaulizia wachezaji watatu, mbali ya Bocco ni Kipre Tchetche na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
    Bocco hakufanya mazoezi leo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti tangu aumie alipogongana na Mbuyu Twite wa Yanga SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Agosti 17 mwaka huu, ambao timu yake ililala 1-0.
    Tunakupenda wewe, lakini sisi Rhino; Watoto wakionyesha upendo kwa Bocco. Kushoto ni Meneja Jemadari Said.

    Na akiwa nje anaangalia mazoezi alifuatwa na watoto walioomba kusalimiana naye na kumsifu kwamba yeye ni mchezaji mzuri na wanampenda sana. 
    Hata hivyo, watoto hao walimuacha hoi Bocco walipomuambia; “Tunakupenda wewe, lakini sisi ni Rhino,”. Bocco akabaki anacheka.
    Rhino inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) imepanda Ligi Kuu msimu huu na kuwa timu ya kwanza ya mkoa huu kucheza Ligi Kuu tangu iliposhuka Milambo ya Tabora mwaka 2001. 
    Kwa kuikosa Ligi Kuu kwa kipindi chote hicho, kwa kiasi kikubwa wana Tabora wameamua kuweka kando itikadi zao na kuungana kuisapoti Rhino idumu Ligi Kuu ili waendelee kuwaona nyota wa soka Tanzania wa timu mbalimbali kupitia ligi hiyo kama Adebayor wa Chamazi.
    Tayari mashabiki wa hapa wametunga wimbo mzuri timu hiyo inapocheza Mwinyi; “Kama siyo Juhudi zako Rhino, Ligi Kuu Tungeiona wapi”.
    Rhino ilianza Ligi Kuu kwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Simba SC Jumamosi, wakati Azam nayo ilitoa sare ugenini 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro. Je, nani ataibuka  mbabe kesho, au ni sare tena?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: WATOTO TABORA WAMUAMBIA BOCCO; "TUNAKUPENDA WEWE, LAKINI SISI NI RHINO" Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top