• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 27, 2013

  HII NDIYO RUFAA YA YANGA KUPINGA ADHABU YA NGASSA

  IMEWEKWA AGOSTI 27, 2013 SAA 3:31 USIKU
  "Klabu ya Yanga ilipokea barua ya TFF ya tarehe 16/08/2013 kuijulisha adhabu iliyotolewa kwa Mchezaji Mrisho Ngasa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF. 
  Barua hiyo inataja adhabu hiyo kuwa nikumfungia Mchezaji Ngasa mechi zipatazo 6 na adhabu ya kulipa sh. 30milioni pamoja na riba ya asilimia 50% yaani 15milioni na kufanya jumla ya shilingi 45milioni. Lakini barua hiyo haitaji kifungu cha Kanuni Yanga au Ngasa aliyokiuka. 
  Yanga inaiona adhabu hii kuwa ni ya uonevu, kwa Klabu na Mchezaji inayokiuka kanuni za mashindano hayo, misingi ya sheria na haki za msingi za mlalamikiwa.
  Mwalusako na Ngassa

  Mnamo tarehe 23/8/2013 Klabu ya Yanga Iliwasilisha rufaa yake TFF kupinga adhabu hiyo, na sababu za rufaa hiyo ni kama ifuatavyo:-

  KAMATI ILIKOSEA KIKANUNI NA KISHERIA KUMWADHIBU NGASA KWA KUZINGATIA MKATABA BATILI
  Suala la usajili wa mchezaji Mrisho Ngasa baina yake na Simba Mara baada ya Msimu wa 2012/2013 kumalizika ulikuwa na matukio makubwa yaliyomhusu Mchezaji Mrisho Ngasa, Klabu ya Simba na Klabu ya Azam. Kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya TFF ilipaswa kuyarejea kabla ya kufikia uamuzi waliofikia hasa kwa kuzingatia mchezaji hakuwepo kujitetea katika kikao hicho.
  Tukio baada ya Mechi kati ya Yanga na Azam Kumalizika katika msimu wa 2012/2013.
  Baada ya mechi hiyo hakuna asiyekumbuka mrisho Ngasa kuonesha mapenzi yake kwa Klabu ya Yanga, baada ya kuvaa jezi ya yanga na kubebwa na mashabiki wa Yanga. 
  Timu ya Azam Kutangaza kumpeleka Ngasa
  Tukio la Ngasa kuvaa Jezi ya Yanga halikuifurahisha Klabu ya Azam na kutoa mapendekezo ya kumtoa kwa mkopo kwa klabu iliyokuwa tayari kutoa kiasi cha dola 50,000, na yanga hawakuafiki kiwango hicho ndipo Simba walifanikiwa kumnyakua Ngasa kwa Mkopo. Na klabu ya Azam iliutangazia umma wa wa Tanzania kumpeleka Ngasa kwa mkopo katika klabu ya Simba. Kamati yako pia inaweza kufuatilia katika mtandao wa Azam fc (  HYPERLINK "http://www.azamfc.co.tz" www.azamfc.co.tz). 

  Tamko la Mrisho Ngasa Kushangazwa na uamuzi huo pasipo kushirikishwa.
  Baada ya umma kutangaziwa uamuzi huo Mchezaji Ngasa alitoa tamko kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari Tamko la Ngasa kutokuwa tayari kuuzwa kama mbuzi, kwani hakushirikishwa. Klabu yake na Simba waliweka msimamo na Ngasa alitishwa kuwa asingeenda Simba basi angekaa benchi mpaka mwisho wa Mkataba wake.

  Uamuzi wa Klabu ya Simba Kumkabidhi Ngassa Gari na Pesa. 
  Baada ya tamko hilo la Klabu ya Azam na Mchezaji Ngasa. Mchezaji huyo ina semekana alitoweka na kufunga mawasiliano yake, lakini baadaye alionekana katika vyombo vya habari vilivyoripoti tarehe 2/8/2012akiwa amepigwa picha akiandika mbele ya Kiongozi wa Simba.  Baada ya sinema hizo Ngasa kwa unyonge alisikika akisema amekubali kucheza Simba. Na tarehe 3/8/2012 Ngasa aliripotiwa katika picha na Vyombo vya habari akiwa mbele ya gari iliyosemekana alipewa na Simba.

  Mkakati wa Azam Fc Kummuza Ngasa Katika Klabu ya Elmerekh
  Ikumbukwe pia kuwa wakati akiwa katika mkataba wa mkopo baina ya simba na Azam, Simba walifanya utaratibu wa kumumsajili Ngasa, usanii ni mnamo tarehe December 5, 2012 vyombo vya habari viliripoti  Azam yamuuza Ngasa kwa Elmereikh kwa $ 75,000 sawa na  Milioni 120
  Suala la kujiuliza ni kwanini Mkataba waliotia Simba wa tarehe 2/8/2012, haukuizuia Azam kumuuza Ngasa December 5, 2012? Jibu ni rahisi kwamba Mkataba haukuwa na nguvu yeyote ya Kikanuni au kisheria kwa maana ya uhamisho na usajili wa wachezaji, ndio maana Simba hawakupinga, lakini Ngasa alikataa na kujificha hata maafisa wa timu hiyo walipofika Tanzania bila kuonana na Ngasa.
  Katika Mwongozo wa FIFA juu ya hadhi za wachezaji na masuala ya kinidhamu (FIFA Manual; Players Status and Disciplinary Matters) kipengele cha 3(d) kinaeleza wazi kuwa katika kuhakikisha uthibiti wa mkataba baina ya mchezaji na klabu, mahusiano ya kiajira lazima yazingatie uwiano baina ya matakwa ya mchezaji na ya klabu (yaani pande zote mbili). 
  Kifungu cha 3(f) cha Mwongozo huo unabainisha kuwa kuna vipindi viwili tu vya usajili, katika msimu mmoja. Swala la kujiuliza Simba waliingia makubaliano na Ngasa katika kipindi kipi mbali na kuwa katika mkopo kwa msimu mmoja?
  Kimsingi Mchezaji Ngasa hakuwa na mkataba halali na Simba inakuwaje Ngasa awajibishwe kinidhamu na Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji kwa makubaliano ambayo hayatambuliwi kikanuni na kisheria?
  Hata kama imebainika kuwa Mrisho Ngasa alikuwa na mkataba na klabu ya Simba, ni wazi kuwa katika maelezo hapo juu hapakuwa na hiari ya mchezaji kuamua kuingia katika mkataba.
  Sheria ya Mikataba ya Tanzaia Sura ya 345 kifungu cha 10 kinatanabaisha kwamba makubaliano yote yanakuwa mkataba kama yamefanyika kwa hiari na uhuru wa  kila upande. Kifungu cha 14 cha sharia hiyo inaongeza kuwa makubaliano yanakuwa ya hiyari endapo yanafanyika pasipokuwa na kulazimishwa au shuruti, pasipo kuwa na shinikizo, pasipokuwa na udanganyifu, au makosa.
  Kifungu cha 19 cha sheria ya mikataba inatanabaisha kuwa pale ambapo hiyari katika mkataba inapatikana pakiwa na kulazimishwa au hiyari ,shinikizo, udanganyifu au makosa basi mkataba huo unakuwa ni batilifu ( voidable) kwa upande ambao hiyari ilipatikana kwa hila hizo hapo katika kifungu cha 19.
  Je katika suala hili endapo Ngasa alipewa fedha na gari kulikuwa na hiyari ya dhati? Ikumbukwe kuwa Ngasa alitishiwa kuwa asipokubali kucheza Simba angekaa benchi hadi mwisho wa mkataba wake.
  Alikubali kuingia mkataba akiwa katika upande dhaifu kimaamuzi/weak position, hata mkataba kama ulikuwepo haukuwa na nguvu kikanuni na kisheria.

  KAMATI ILIKOSEA KIKANUNI NA KISHERIA KUTOA UAMUZI KWA USHAHIDI WA UPANDE MMOJA PASIPO KUMSIKILIZA MRISHO NGASA.
  Ngasa hakupewa nafasi ya kujitetea juu ya utata wa yanayosemekana makubaliano ya  kumpa fedha, Ngasa anaelewa fika alikuwa kwa mkopo Simba, na kwamba simba hawakuwa na uwezo kwa kanuni za usajili kumpa mkataba wa usajili kwa wakati huo, suala hilo lingepata majibu mazuri kama ngasa naye angepewa fursa ya kuelezea alivyouelewa mkataba huo.
  Ngasa hakuitwa, hivyo alinyimwa haki ya msingi ya kusikilizwa. Kamati ilithibitisha vipi tuhuma za kupokea fedha na kufikia kutoa adhabu kali kama ile ya kurudisha milioni 45 pasipo mtuhumiwa kusikilizwa?
  Na kama ilithibitisha Ngasa kupokea fedha ni kiasi gani? Na kama alipewa gari thamani yake ni kiasi gani, hivyo vyote huthibitishwa kwa  risiti au bank statement.
  Hata Kanunu za adhabu za FIFA katika kifungu cha kinasisitiza kabla ya kutoa adhabu lazima mlalamikiwa apewe fursa ya kusikilizwa.
  Haya mambo yote yalipaswa kupatiwa majibu kabla ya kutoa uamuzi na adhabu kwa Yanga na Ngasa, kwa kutopata maelezo ya Mchezaji, Kamati  imemnyima  Ngasa haki ya msingi ya kusikilizwa kabla ya Kuadhibiwa  (Aud auteram patem) -the right to be heard, wala hapakuwa na mtu wa kumtetea.

  KAMATI ILIKOSEA KIKANUNI KUMWADHIBU MCHEZAJI MRISHO NGASA KWA KUINGIA MKATABA NA SIMBA NJE YA KANUNI ZA USAJILI.
  Hakuna shaka Simba ilimrubuni mchezaji kwa kumshawishi asaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo nje ya utaratibu wa usajili na bila woga waliuleta mkataba huo na kuweka pingamizi.
  Hata kanuni za FIFA zimeweka adhabu kali kwa viongozi wanao gushi nyaraka za kuweka mahusiano ya kisheria kama inavyodaiwa na Simba dhidi ya Ngasa, kwa kuwa uhalali wa mkataba huo unatia mashaka kwa mujibu wa kanuni za usajili na adhabu hutolewa kwa mujibu wa  Chapter II, Section 5 Article 61 ya Kanuni za Adhabu za Fifa (FIFA Disciplinary code) ina tamka wazi kuwa endapo kutakuwa na udanganyifu au kugushi nyaraka zinazo husiana na shughuli za mpira ikiwa aliyefanya hayo ni kiongozi adhabu yake ni kufungiwa kwa uchache miezi 12.
  Pia endapo Klabu imekiuka taratibu za usajili kama zilivyowekwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 na 6 vya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa wachezaji za fifa na TFF.
  Je endapo alipewa fedha na gari je ilikuwa ni kwa ajili ya Usajili wa msimu huu au kuridhia kucheza kwa mkopo akiwa mchezaji wa Azam.
  Na kama ilikuwa ni kwa ajili ya usajili wa Msimu huu kwa nini Azam FC tarehe 5/8/2012 waliamua kumuuza Ngasa Sudani na bila Simba kuleta malalamiko rasmi TFF?
  Je mkataba ulikuwa ni wa kuichezea Simba kwa msimu huu wa 2013/2014, mkataba huo ulifanyika katika kipindi mahsusi cha kuingia mkataba na mchezaji au ni makubaliano ya awali (MOU), kama ni makubaliano ya awali kamati hiyo haikupaswa kujihusisha na makubaliano hayo. Kwa namna yeyote ile mkatabawa Simba na Ngasa wa tarehe 2/8/2012 ulifanyika ndani ya mkataba wa mkopo na Azam na hivyo mkataba wa Simba ukawa batili na ndivyo kamati ilivyoona.
  Je, kamati ilifanya sahihi kuutambua mkataba huo pasipo kumuuliza mchezaji na kuamuru kurudisha fedha na fidia isiyo ya haki wakati kamati haitambui uhalali wa mkataba huo? 
  Kama vile kamati iliona haikuwa halali kuiadhibu Simba hivyo hivyo haikuwa na mamlaka kikanuni kutoa adhabu kwa Ngasa kwa mujibu wa majukumu yaliyo ainishwa katika Kipengele cha 40(8) cha Katiba ya TFF.

  KAMATI ILIKOSEA KISHERIA KWA WALIOWEKA PINGAMIZI KUWA SEHEMU YA KUTOA UAMUZI
  Kamati imekiuka haki ya msingi inayomzuia mtu kuwa jaji kwenye shauri lake mwenyewe.(“Nemo Judex in causa sua”)
  Kama tulivyoeleza hapo awali, Simba ndio walioweka pingamizi na tuhuma za mkataba na viongozi wa Simba walikaa katika kamati iliyoamua hatma ya Ngasa pasipo Ngasa kuwakilishwa kwa vyovyote maamuzi hayangemtendea haki Ngasa. 

  KAMATI ILIKOSEA KIKANUNI KUINYIMA KLABU YA YANGA KUMTUMIA NGASA KATIKA MECHI SITA PASIPO NA SABABU ZA MSINGI.
  Kwa kumfungia Ngasa mechi sita ni kuiadhibu Klabu ya Yanga kwa kosa ambalo kama lipo haijahusika nalo, Klabu ya yanga imemsajili Ngasa kihalali hivyo kumfungia Ngasa ni uonevu kwa Yanga. 
  Haikubaliki kimantiki kutomruhusu Ngasa kuchezea Yanga wakati huo huo TFF wanamtumia katika Timu ya taifa, kama ambavyo TFF/Timu ya Taifa haihusiki katika mkataba batilifu, Yanga nayo haihusiki na makosa yeyote, hivyo ni uonevu kwa Yanga kutomruhusu Ngasa kuitumikia katika mechi sita. 
  Ni rai yetu nyenyekevu Kuomba kamati yako kuifutia Yanga adhabu ya kutomtumia mchezaji Ngasa katika mechi tano zilizosalia, kwa kuwa katika suala hili Yanga anakuja mbele ya kamati yako akiwa na mikono safi.
  Katibu Mkuu
  Young Africans SC.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: HII NDIYO RUFAA YA YANGA KUPINGA ADHABU YA NGASSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top