• HABARI MPYA

  Monday, October 23, 2023

  AZIZ KI APIGA HAT TRICK YANGA YAICHAPA AZAM FC 3-2 NA KUREJEA KILELENI LIGI KUU


  MABINGWA watetezi, Young Africans wameibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
  Ilikuwa siku nzuri kwa kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki aliyefunga mabao yote matatu ya Yanga leo.
  Bao la kwanza alifunga dakika ya nane akimalizia pasi ya Nahodha, Bakari Nondo Mwamnyeto, la pili akafunga dakika ya 69 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya yeye mwenyewe kuchezewa rafu umbali wa mita 22 na la tatu akafunga dakika ya 72 akimalizia pasi ya kiungo Mganda, Khalid Aucho.
  Azam FC iliyotanguliwa, ilisawazisha kupitia kwa beki Msenegal, Gibrill Sillah dakika ya 19, kabla na wao kutangulia kwa bao la mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo kwa penalti dakika ya 62.
  Refa Ahmed Arajiga aliyetenga mkwaju huo wa penalti baada ya beki Mwamnyeto kumchezea rafu Djibrill Sillah kwenye boksi.
  Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 15 katika mchezo wa sita na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi tu wastani wa mabao Simba SC ambayo pia ina mchezo mmoja mkononi, wakati Azam FC inayobaki na pointi zake 13 za mechi sita pia inashukia nafasi ya tatu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZIZ KI APIGA HAT TRICK YANGA YAICHAPA AZAM FC 3-2 NA KUREJEA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top