• HABARI MPYA

    Saturday, March 07, 2026

    YANGA SC YAIANDIKIA BODI YA LIGI ‘WARAKA MZITO’ DHIDI YA MWALIMU NA KAMATI YA SAA 72


    KLABU ya Yanga imeiandikia barua Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TBLB) kuomba ufafanuzi wa kina juu ya adhabu iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya TPLB, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kwa mchezaji Suleiman Abdallah Mwalimu kufungiwa mechi tatu badala ya tano kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine watano waliofanya makosa kama kama yake.
    Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ally Shaaban Kamwe amesema kwamba wanahitaji Bodi iweke bayana kuna upekee gani wa tukio la Mwalimu lililoifanya Kamati ya saa 72 kutumia kanuni tofauti ya 41:5(5.2) na wengine watano kutumika kanuni ya 41:21.


    “Jambo la pili, tumeitaka Bodi ya Ligi itoe ufafanuzi kwanini kamati ya saa 72 ilichelewa kukutana kama kanuni zinavyoelekeza ili kufanya mapitio ya makosa mbalimbali na kutoa hukumu kwa waliobainika ikiwemo tukio la mchezaji Selemani Mwalimu. Aidha mechi zingine zilizopita Kamati hii ya saa 72 ilikutana kwa wakati na kutoa hukumu. Kulikuwa na changamoto gani iliyopelekea kucheleweshwa kwa haki,”” amesema Ally Kamwe.
    “Jambo la tatu, Kamati ya saa 72 imetoa hukumu kwa waamuzi wasaidizi 1&2, kwenye mchezo wa Yanga SC dhidi ya Simba SC baada ya kushindwa kutafsiri sheria namba 11 [OFFSIDE]. Waamuzi hao wamehukumiwa kwa kanuni moja ya 42:1(1.8) lakini mmoja amefungiwa miezi 6 na mwingine miezi 3. Tunataka tujue ni SAYANSI gani imetumika hapa kuchanganua adhabu hizi kuwa tofauti ikiwa wote wamefanya kosa la kushindwa kutafsiri sheria moja. Je kamati yetu inayo SAYANSI ya kuona kesho kwa kubaini kuwa Prince Dube asingefunga nafasi ya wazi aliyopata?” 
    “Jambo la nne, Kwa mujibu wa sheria za FIFA, goli halali ni lile goli pekee ambalo limeruhusiwa na mwamuzi wa kati. Kinyume na hapo hakuna kamati wala sheria au kanuni ambayo inayo mamlaka ya kuhalalisha goli ambalo halikuidhinishwa na mwamuzi wa kati . Kauli ya kwamba Simba wamenyimwa goli HALALI imeleta taharuki kwa UMMA. Tumeiandikia Kamati itueleze imetoa wapi Mamlaka ya Kutangazia Umma kuwa Goli ni Halali?” 
    “Jambo la tano, kwenye mchezo wa KMC FC dhidi ya Simba SC, Seleman Mwalimu alifunga bao akiwa katika eneo la kuotea. Kamati iliyosema kuna goli halali limefungwa limekataliwa, ilikuwa bubu kusema kuna goli lisilokuwa halali limekubaliwa, aidha hata mwamuzi msaidizi hakufungiwa kama ambavyo waamuzi wasaidizi wamefungiwa kwenye mechi ya Derby” Ally Kamwe 
    “Mechi nyingi za Yanga SC kukiwa na makosa yanayohusisha sheria namba 11 (Kuotea/Offside), kamati hii imekua makini sana kufanya maamuzi ya kuwafungia waamuzi. Lakini matukio hayo yakiwa yanaiumiza Yanga kamati hii imegeuka kuwa bubu. Mfano mchezo wa Yanga dhidi ya JKT mwamuzi Glory Tesha alizuia matukio mawili ya wazi ya Yanga kufunga kwa madai kuwa wachezaji wetu waliotea. Lakini kwa marejeo ya video iliyonekana kuw Wachezaji hawa hawakuwa kwenye eneo la Kuotea, Mpaka sasa kamati haijachukua maamuzi kwa waamuzi husika” 
    “Mwisho na kwa umuhimu, hii ni klabu ya wanachama, wanahitaji kujua taarifa za timu yao. Bodi ya ligi ikijibu tutakuja kuwaeleza wanachama tulichojibiwa. Na wasipojibu tutakuja kuwajuza wanachama wetu kwamba hatujajibiwa,”amemalizia Kamwe.


    Hatua hii ya Yanga inafuatia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya TPLB kuwafungia marefa wote wasaidizi katika mechi ya watani wa jadi ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Kassim Mpanga wa Dar es Dalaam na Hamdani Said wa Mtwara wote wamefungiwa kwa makosa yanayofanana, kutotafsiri kwa usahihi sheria.
    Mwamuzi Msaidizi namba moja, Mpanga amefungiwa miezi sita kwa kukataa bao la Simba SC lililofungwa na mshambuliaji Suleiman Abdallah Mwalimu dakika ya 70, wakati Hamdani amefungiwa miezi mitatu kwa kuzima shambulizi la hatari la Yanga alipomuinulia kibendera cha kuotea mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Mpumelelo Dube dakika ya 61.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Nassor Mwinchui wa Tanga Jumapili iliyopita, Machi 1Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar – miamba hiyo ya Kariakoo ilitoshana nguvu kwa sare ya bila mabao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAIANDIKIA BODI YA LIGI ‘WARAKA MZITO’ DHIDI YA MWALIMU NA KAMATI YA SAA 72 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top