• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 15, 2019

  AZAM FC YA IDDI CHECHE YAENDELEA KUTOA VIPIGO VIKALI, YAICHAPA SINGIDA UNITED 4-0

  Na Mwandishi Wetu, DAR SALAAM
  TIMU ya Azam FC imeendelea kufanya vyema chini ya kocha wake wa muda, Iddi Nassor ‘Cheche’ baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Singida United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Nyota ya mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Dombo Ngoma imeendelea kung’ara leo baada ya kufunga mabao mawili katika dakika za 77 na 90, huku mabao mengine yakifungwa na viungo wazawa, Ramadhani Singano ‘Messi’ dakika ya 66 na Joseph Mahundi dakika ya 74.
  Kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 59 baada ya kucheza mechi 28, ingawa inabaki nafasi ya pili nyuma ya vinara, Yanga SC wenye pointi 67 za mechi 27 na mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 51 za mechi 20.
  Katika mechi zilizotangulia jioni ya leo, Tanzania Prisons nayo imeendelea kufanya vyema chini ya kocha wake mpya, Mohammmed Rishard ‘Adolph’ baada ya kuichapa 2-0 JKT Tanzania Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

  Pongezi kwa wafungaji wa mabao hayo katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua Vedastus Mwihambi na Adam Adam.
  Na kwa ushindi huo, Tanzania Prisons inafikisha pointi 38 baada ya kucheza mechi 30 na kujiinua kutoka nafasi ya 12 hadi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu inayoshirikisha timu 20.
  Hali ni mbaya kwa JKT Tanzania iliyocheza mechi ya kwanza leo tangu imsimamishe kocha wake, Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ wiki iliyopita, kwani inabaki na pointi zake 36 baada ya kucheza mechi 31 na inateremka kwa nafasi mbili hadi ya 14.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo,  Stand United wameibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex huko Kishapu mkoani Shinyanga.
  Mabao ya Stand United yamefungwa na Datius Peter na Jacob Masawe, wakati bao pekee la Mwadui FC limefungwa na Salim Aiyee.
  Stand United inafikisha pointi 36 baada ya ushindi huo katika mechi 31 na kujiinua hadi nafasi ya 11 kutoka ya 17, wakati Mwadui FC inateremkia nafasi ya 10 ikibaki na pointi zake 36 za mechi 31.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tano zaidi, Lipuli FC wakiikaribisha Yanga SC Uwanja wa Samora mjini Iringa, Coastal Union wakiwa wenyeji wa Alliance FC Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Biashara United na African Lyon Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Mbeya City dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YA IDDI CHECHE YAENDELEA KUTOA VIPIGO VIKALI, YAICHAPA SINGIDA UNITED 4-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top