• HABARI MPYA

  Saturday, March 16, 2019

  TP MAZEMBE, ESPERANCE ZAFUZU ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA

  TIMU ya Al Ahly ya Misri imefuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama kinara wa Kundi D kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura usiku huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria nchini Misri.
  Ushindi huo umetokana na mabao ya Fateh Talah aliyejifunga dakika ya 30, Marwan Mohsen dakika ya 45 na ushei na Hussein El Shahat dakika ya 81.
  Kwa matokeo hayo, Ahly inamaliza kileleni mwa Kundi D kwa pointi zake 10, ikifuatiwa na Simba SC yenye pointi tisa, wakati JS Saoura ni ya tatu kwa pointi zake nane na AS Vita imeshika mkia kwa pointi zake saba.
  Mechi nyingine ya Kundi D leo, Simba SC imefanikiwa kwenda Robo Fainali baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) usiku huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

  Shujaa wa Simba SC leo ni kiungo Mzambia, Clatous Chama aliyefunga bao la ushindi dakika ya 90 akimalizia pasi ya Nahodha, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, John Raphael Bocco aliyesogeza krosi ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Niyonzima.
  Na hiyo ilifuatia AS Vita kutangulia kwa bao la Francis Kazadi Kasengu dakika ya 12 akimalizia mpira uliozuiwa na beki Muivory Coast wa Simba SC, Serge Wawa Pascal baada ya shuti la Fabrice Ngoma.
  Ikawachukua Simba SC dakika 24 kusawazisha bao hilo kupitia kwa beki wake wa kushoto na Nahodha Msaidizi wa klabu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyewazidi mbio mabeki wa AS Vita dakika ya 36 baada ya kutanguliziwa pasi na kiungo Muzamil Yassin.
  Mechi nyingine za leo, Esperance imeshinda 2-1 ugenini dhidi ya Platinum, Club Africain imeichapa 1-0 Ismailia, TP Mazembe imeichapa 2-0 CS Constantine, Wydad Casablanca imeichapa 1-0 Mamelodi Sundowns, Lobi Stars imeichapa 2-0 ASEC Mimosas na Horoya imeichapa 2-1 Orlando Pirates.
  Mbali na Al Ahly na Simba SC kutoka Kundi D, timu nyingine zilizofuzu Robo Fainali ni kutoka Kundi A Wydad Casablanca ya Morocco na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Kundi B Esperance ya Tunisia na Horoya ya Guinea, Kundi C TP Mazembe ya DRC na CS Constantine ya Algeria.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TP MAZEMBE, ESPERANCE ZAFUZU ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top