• HABARI MPYA

  Friday, March 29, 2019

  AZAM FC YATINGA NUSU FAINALI KOMBE LA TFF BAADA YA KUIPIGA 1-0 KAGERA SUGAR KAITABA

  Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
  TIMU ya Azam FC imetinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera.
  Ushindi huo muhimu unaifanya Azam FC kukutana KMC katika hatua hiyo, mchezo unaotarajia kupigwa Uwanja wa Azam Complex mwezi Mei mwaka huu, ambapo wapinzani wao hao wametinga nusu fainali baada ya kuichapa African Lyon mabao 2-0.
  Azam FC ililazimika kusubiri hadi dakika ya 79 kuweza kujipatia bao hilo la ushindi lililofungwa kiustadi na winga Joseph Mahundi, aliyetumia vema pasi ya mpenyezo ya kiungo mkabaji, Stephan Kingue.
  Joseph Mahundi akipongezwa na Mzimbabwe, Bruce Kangwa baada ya kuifungia bao pekee Azam leo 

  Mechi hiyo ilikuwa na ushindani mkubwa, ambapo Azam FC ilijitahidi kufanya majaribio kadhaa kupitia kwa washambuliaji wake, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na kiungo Mudathir Yahya kabla ya kupata bao hilo.
  Azam FC ililazimika kucheza pungufu dakika 23 za mwisho za mchezo huo, baada ya kipa Razak Abalora, kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Shomari Lawi, baada ya kumfanyia madhambi mchezaji wa Kagera Sugar aliyekuwa akienda kufunga bao.
  Baada ya kadi hiyo nhyekundu, benchi la ufundi la Azam FC lililazimika kumfanyia mabadiliko mshambuliaji Obrey Chirwa na kumwingiza kipa Mwadini Ally, ili akazibe pengo hilo la Abalora.
  Mara baada ya mchezo huo kikosi cha Azam FC kinatarajia kuelekea mkoani Mwanza kesho Jumamosi asubuhi tayari kukipiga tena na Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaopigwa Uwanja wa Nyamagana Aprili 3 mwaka huu.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razak Abalora, Nicolas Wadada, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda, Aggrey Morris, Stephan Kingue, Joseph Mahundi, Mudathir Yahya/Frank Domayo dk63, Donald Ngoma, Obrey Chirwa/Mwadini Ally dk69, Ramadhan Singano/Enock Atta Agyei.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YATINGA NUSU FAINALI KOMBE LA TFF BAADA YA KUIPIGA 1-0 KAGERA SUGAR KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top