• HABARI MPYA

  Saturday, March 23, 2019

  KILA MCHEZAJI KUPEWA SH MILIONI 10 TAIFA STARS IKIIFUNGA UGANDA NA KUFUZU AFCON

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametembelea kambi ya timu ya taifa hoteli ya Bahari Beach mjini Dar es Salaam leo huku ahadi ikitolewa iwapo Tanzania itafuzu Fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Juni mwaka huu nchini Misri, kila mchezaji atapatiwa bakhshishi ya Sh. Milioni 10.
  Katika ziara yake hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa amewaambia wachezaji kwamba Serikali na wananchi wana matumaini makubwa kwa timu yao, hivyo wahakikishe wanapata ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda.
  Majaliwa ambaye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Uganda, amewataka wachezaji hao wasiwe na wasiwasi kwa sababu hawana tofauti yoyote na wachezaji wa timu nyingine duniani.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta leo mjini Dar es Salaam

  “Macho yote ya Watanzania yameelekezwa katika mechi ya kesho na Serikali ina matumaini makubwa na timu ya Taifa, hivyo waelewe kwamba kesho ni siku muhimu sana. Lengo letu ni kufikia hatua ambayo mataifa mengine yamefikia” amesema.
  Taifa Stars itakuwa mwenyeji wa Uganda, The Cranes kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi L kufuzu AFCON 2019 kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Mechi hiyo itachezeshwa na marefa kutoka nchini Gabon ambao ni Eric Arnaud Otogo Castane atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Moussounda Montel na Marlaise Ditsoga Boris.
  Mechi nyingine ya Kundi L kesho kati ya Cape Verde na Lesotho mjini Praia itachezeshwa na refa Mahamadou Keita atakayesaidiwa na washika vibendera Baba Yomboliba na Nouhoum Bamba, wote wa Mali mjini Praia.
  Tanzania inayofundishwa na kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike inahitaji ushindi Jumapili ili kuangalia uwezekano wa kufuzu AFCON ya Juni nchini Misri iwapo Lesotho itafungwa au kutoa sare na Cape Verde.
  Kihistoria, Tanzania imeshiriki AFCON moja tu mwaka 1980 nchini Nigeria baada ya kuitoa Zambia katika raundi ya mwisho ya mchujo kwa ushindi wa jumla wa 2-1, ikishinda 1-0 Dar es Salaam na kutoa sare ya 1-1 mjini Ndola. 
  Awali ya hapo, Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema kwamba kamati yake itatoa Sh. Milioni 10 kwa kila mchezaji wa timu hiyo itaifunga Uganda kesho katika mchezo wa mwisho wa Kundi L na kufuzu AFCON ijayo nchini Misri.
  Makonda amesema Watanzania wanachokijua kwa sasa ni kwamba AFCON 2019 ni zamu yao, hivyo amewaomba wachezaji wa timu ya Taifa wahakikishe wanawapa furaha kwa kuifunga timu ya Taifa ya Uganda na kwamba wananchi wengi wamehamasika kwenda kuwashangilia.
  Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangala ameahidi kuwapeleka katika mbuga ya wanyama kwa ajili ya mapumziko iwapo wachezaji hao wataibuka na ushindi katika mechi yao dhidi ya Uganda kesho.
  Dk. Kigwangala amesema Serikali ipo pamoja na wanamichezo, ambapo amewataka wachezaji hao wa timu ya Taifa wakapigane kweli kweli kwa ajili ya Taifa lao. “Kesho muingie uwanjani kama askari wa nchi. Mkapiganie ushindi wa Taifa letu”.
  Awali, Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samata alisema; “Ninafuraha si kwa sababu ya ukubwa wa mechi ya kesho bali ni kwa sababu naona kesho nakwenda kuongoza nchi. Tupo tayari kuliletea Taifa ushindi”.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA MCHEZAJI KUPEWA SH MILIONI 10 TAIFA STARS IKIIFUNGA UGANDA NA KUFUZU AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top