• HABARI MPYA

  Wednesday, March 27, 2019

  KAPTENI MKUCHIKA AUNDA KAMATI MBILI YANGA, APENDEKEZA UCHAGUZI MKUU APRILI 28

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BARAZA la Wadhamini la klabu ya Yanga leo limeunda Kamati ya Usimamizi wa timu, chini ya Mwenyekiti, Mashauri Lucas na Makamu wake, Said Ntimizi.
  Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya viongozi wawili waliobaki madarakani Yanga kujiuzulu leo na kukabidhi timu kwa Baraza la Wadhamini chini ya Mwenyekiti, Kapteni George Huruma Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani mjini Dar es Salaam, Kapteni George Huruma Mkuchika amewataja Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa timu ni Hussein Ndama na Wajumbe, Samuel Lukumay, Hussien Nyika, Moses Katabaro na Maulid Kitenge.

  Aidha, Mkuchika aliyeongozana na Makamu wake, Mama Fatma Karume, mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume (sasa maremeu) amesema kwamba Baraza limependekeza Uchaguzi Mkuu wa Yanga ufanyike Jumapili ya Aprili 28, mwaka huu.
  Na Mkuchika akataja majina ya wajumbe 10 watakaounda Kamati ya Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo, ikichanganya wajumbe wanne waliopendekezwa na wabunge ambao ni mashabiki wa timu hiyo, huku wajumbe sita wakiwa ni miongoni mwa wale walioteuliwa awali na klabu hiyo. 
  Hao ni Mwenyekiti Samuel Mapande, Daniel Mlelwa, Mustafa Nagal, Geoffrey Mapunda, Edward Mwakingwe, Samuel Mangesho, Issa Gavu, Venance Mwamoto, Seif Gulamali na Dunstan Kitandula.
  Baadaye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alifika makao makuu ya Yanga na kufanya mazungumzo na Baraza la Wadhamini na akasema ameridhishwa na hatua zilizochukuliwa. 
  Mapema leo asubuhi, Viongozi wawili waliokuwa wamebaki madarakani Yanga SC, kaimu Mwenyekiti Samuel Lukumay na Mjumbe, Hussein Nyika walitangaza kujiuzulu nafasi zao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam ili kupisha mchakato wa uchaguzi mkuu wa klabu hiyo.
  Lukumay amesema wamelazimika kujiuzulu baada ya Wajumbe wenzao wawili, Siza Lyimo na Thobias Lingalangala kujiuzulu wiki mbili zilizopita na kufanya klabu ibaki na viongozi wawili tu  kati ya 13 waliochaguliwa katika uchaguzi wa juni 12, mwaka 2016 Dar es Salaam, ambao ni yeye na Nyika.
  “Kikubwa kilichotusababihsa tufanye hivi, ni kwamba nadhani wiki moja mbili zilizopita, tulikuwa tumebaki wajumbe wanne, lakini wenzetu wawili walijiuzulu hiyvo uchaguzi mdogo ungekuwa wa kujaza nafasi sita,”amesema Lukumay. 
  Amesema sasa Baraza la Wadhamini na Sekretarieti ya klabu watashirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuendesha mchakato wa Uchaguzi Mkuu ambao unaanza upya.  
  Wengine waliojiuzulu ni Mwenyekiti Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe Inspekta Hashim Abdallah, Salum Mkemi, Omary Said na Ayoub Nyenzi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAPTENI MKUCHIKA AUNDA KAMATI MBILI YANGA, APENDEKEZA UCHAGUZI MKUU APRILI 28 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top